Rais Zelensky amtaka Trump aitembelee Ukraine  kabla ya kufanya mazungumzo na Urusi

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ametoa wito kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, kuitembelea Ukraine na kushuhudia kwa macho yake athari za uvamizi wa Urusi kabla ya kuunga mkono au kukubaliana na pendekezo lolote la amani kutoka kwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Katika mahojiano maalum na kituo cha televisheni cha CBS cha Marekani, Zelensky alisema kuwa ni muhimu kwa Trump kuona mateso na uharibifu uliosababishwa na vita vinavyoendelea, akimtaka atembelee hospitali, makanisa yaliyoharibiwa, na kukutana na waathirika wakiwemo watoto waliopoteza maisha au kujeruhiwa.

“Naomba aje. Aje aone anachotaka kuona. Kama ana muda, aje Sumy, aje Kyiv, aje sehemu yoyote ile,” alisema Zelensky katika mahojiano hayo.

Kauli hiyo ya Zelensky ilitolewa wakati taifa hilo likikumbwa na mashambulizi mapya kutoka kwa Urusi, ambapo roketi zilirushwa katika mji wa Sumy na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 34, pamoja na kujeruhi wengine wengi. Taarifa kutoka kwa huduma za dharura za Ukraine zinasema kuwa juhudi za uokoaji zinaendelea huku hofu ya mashambulizi zaidi ikitanda.

Hii si mara ya kwanza kwa Zelensky kumtaka Trump kuelewa kwa undani hali halisi ya vita hiyo, lakini ni mara ya kwanza kutoa mwaliko wa moja kwa moja wa kutembelea maeneo yaliyoathirika.