Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla leo Ijumaa Agosti 29, 2025 ameeleza kuwa katika Uongozi wake Mkoani Arusha pamoja na mambo mengine atahakikisha Mkoa wa Arusha unapata timu ya Mpira wa miguu kwaajili ya kushiriki Ligi Kuu kama sehemu ya kukuza vipaji vya Vijana na uchumi wa Mkoa wa Arusha.
Mhe. Makalla ameyaeleza hayo wakati wa hafla ya Mapokezi yake Mkoani Arusha, akisema uwepo wa timu ya Mpira wa Miguu Mkoani Arusha ni miongoni mwa chachu nyingine itakayokuza utalii wa Michezo, ikienda sambamba na ujenzi wa uwanja wa AFCON unaoendelea kwenye Kata ya Olmot, Halmashauri ya Jiji la Arusha kwaajili ya kutumika kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika itakayochezwa mwaka 2027 kwa ushirikiano wa uenyeji wa Tanzania, Kenya na Uganda kwa pamoja.
“Inasikitisha Mkoa wa Arusha pamoja na utalii na mambo mengine na tunaenda kujenga uwanja wa AFCON na mna viwanja vizuri lakini Arusha hamna timu hata moja ya ligi kuu. Kuna kitu kinaitwa Utalii wa michezo (Sport Tourism) mtakuwa na uwanja wa michezo bila timu ya ligi kuu?

“Lazima tuwe na utalii wa michezo, kukiwa na timu ya ligi kuu hapa tutachangamsha mkoa huu, akina mamalishe watalisha watu, bodaboda watafaidika, wenye mahoteli watafaidika kwani watalii na wageni watakuja Arusha mbali ya utalii mwingine lakini pia tukiwa na timu, kwahiyo mimi ni mwanamichezo, nitaona aibu sana Arusha ambayo Makalla yupo hamna michezo.” Ameongeza kusema Mhe. Makalla.
Katika hatua nyingine Mhe. Makalla pia amesisitiza umuhimu wa wananchi wa Mkoa wa Arusha kuwa walinzi wa amani na utulivu nchini, akisema amani imekuwa msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii na hata fedha zinazoingia Mkoani Arusha kupitia sekta ya utalii isingewezekana kama Arusha isingekuwa na amani na utulivu.
Leave a Reply