Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amefanya ziara Makao makuu ya Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) leo Januari 9, 2025 ambapo amepata taarifa ya utendaji kazi, pia amepata fursa ya kupanda treni ya ‘Mwakyembe’ inayofanya safari zake kutoka stesheni ya TAZARA-Dar es Salaam hadi Pugu-Mwakanga takribani umbali wa zaidi ya kilomita 18 kutoka TAZARA stesheni.
Naibu Waziri Kihenzile amesema kuwa lengo kubwa la ziara hiyo ambayo ni utekelezaji wa Maelekezo ya Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa ni kuona maendeleo ya utendaji wa treni hiyo inayotoa huduma kwa kazi wa Dar es Salaam pamoja na kujadiliana na Menejimenti ya TAZARA kwa changamoto ambazo zinaweza kupatiwa ufumbuzi wakati ambao Serikai iko katika hatua mbalimbali za kufanya maboresho makubwa katika shirika hilo.
Pia, Naibu Waziri Kihenzile amesema kuwa TAZARA imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika usafirishaji wa abiria na mizigo ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania ambapo takwimu zinazonyesha kwa treni ya Mwakyembe peke yake kwa kipindi cha miaka mitatu iliyo pita mwaka 2021 hadi 2024 imeweza kuhudumia abiria takribani milioni 5 na laki nne.
“Idadi hiyo inaonyesha umuhimu wa moja kwa moja wa kufanya maboresho makubwa yatakayohusisha miundombinu (njia ya reli), vitendea (vichwa na mabehewa) pamoja na majengo (stesheni).” – Naibu Waziri David Kihenzile.
Leave a Reply