NA KELVIN LYAMUYA
NIMEZITAZAMA takwimu za Ligi Kuu Bara na zimenithibitishia kwamba Fountain Gate ni klabu namba nne kwa kufunga mabao mengi msimu huu nyuma ya Yanga Simba na Azam.
Mfungaji wao namba moja ni Selemani Mwalimu ‘Gomez’ halafu wanafuatia wengine wawili na January hii Fountain Gate wamemuuza Mwalimu kwenda Wydad Casablanca ya Morocco.
Selemani ameingia pale Wydad anamkuta mfungaji wao bora kwenye ligi, Mohamed Rayhi akiwa na magoli 8 tu halafu ni straika mwenye umri wa miaka 30, ni mkubwa kwa Sele zaidi ya miaka 10.
Wanaomfuata Rayhi hawafikii hata magoli 6 aliyofunga Sele hapa Tanzania na asilimia kubwa ni viungo. Kwa maana kijana wetu ametua Morocco na jukumu la kwanza ni kuendeleza alichokifanya Fountain Gate, hiyo ni motisha ya kwanza itakayomsaidia.
Kabla ya kuitumia hiyo motisha, kuna hali inayoendelea ndani ya Wydad ambayo inaweza kuifanya motisha yenyewe kuwa chungu na kijana wetu akapotea kwenye ramani ghafla!
Wydad bado wanasumbuliwa na migogoro ndani ya uongozi. Ni hali ambayo imeitikisa klabu kwa kiasi kikubwa na anayenyooshewa sana vidole ni rais wa sasa wa klabu hiyo, Hicham Ait Menna sawa na ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Abdelmajid Bernaki ambaye naye alipata Urais katika kipindi kigumu mno.
Tangu msimu wa 2021/2022 ambao ndio ulikuwa msimu wa mwisho kwa Wydad kubeba kombe la Ligi ya Morocco al-maarufu Botola Pro, mashabiki wa klabu hiyo wamekuwa wakilalamikia mno suala la klabu yao kufanywa mtaji na watu wa pembeni kuliko kuilinda heshima ya kubeba makombe ambayo ndio imelilinda jina la Wydad ndani ya Morocco na Afrika kwa ujumla.
Kimsingi Wydad ilihitaji kiongozi mwenye uwezo wa kutumia njia za kisayansi katika kurudisha muundo imara ndani ya klabu. Kuuchimba mzizi wa matatizo yaliyosababisha mgogoro husika ili klabu irudi katika mstari. Sio Ait Menna wala El Bernaki, hakuna aliyeweza kufanya hivyo.
Katika kipindi cha mwanzo cha uongozi wake, Ait Menna alikuwa na bahati ya kujionea wazi namna gani Wydad ilivyo dhaifu katika mfumo wa kiuongozi ambao umeitafuna taasisi hiyo kubwa kisoka nchini Morocco katika miaka ya hivi karibuni.
Ait Menna angeheshimika zaidi kwa kuweka mezani mipango ya kutatua changamoto hizo na kuzika mgogoro sambamba na kuiinua tena Wydad ambayo imeanza kushuka chini.
Lakini, bosi huyo aliamua kuanza kutafuta matokeo uwanjani kwa kuipa nguvu zote kitengo cha usajili. Hali imekuwa mbaya kiasi kwamba kila usajili unaofanyika hivi sasa hapo Wydad unaonekana ni wa kiwango cha chini!
Hapa kuna mlango ambao Sele anaweza akautumia kutoroka kutoka kwenye presha na kuingia katika chumba cha mafanikio. Sele anaweza akawa mwokozi kwa bwana Ait Menna ambaye katika uongozi wake anaonekana kufeli.
Sele anaweza akawaziba mdomo wale wanaobeza harakati za Rais Ait Menna, anaweza akaitumia silaha yake ya kufunga magoli na kudhihirisha kiongozi huyo alikuwa sahihi kuanza na mpango wa maingizo mapya ya wachezaji, tena wale ambao wanaonekana hawalingani na hadhi ama historia ya Wydad.
Tofauti na hapo, mtifuano unaoendelea ndani ya Wydad unaweza ukampoteza mazima Sele na kwa sababu maisha yake hapo Morocco yatakuwa ni yenye majaribu ikiwemo kutopata nafasi ya kucheza na sababu nyinginezo, huenda akiondoka Wydad asipate timu nyingine nje ya Tanzania halafu kwa masikitiko makubwa tuseme kijana wetu ameshindwa.
Katika lugha takatifu ya soka, ni dhambi kusema atafeli. Na kwanini afeli? Kwanini awape kauli Wanazi wa Wydad ambao wanaamini uongozi wa klabu hiyo umejaa wapigaji na matapeli ambao kwa madai yao, ni kwamba wanawaletea wachezaji wabovu na ambao hawana hadhi ya kuitetea nembo ya Wydad.
Huenda wanazi hao wakawa na hoja maana Wydad mwanzoni mwa msimu huu walianza vibaya mno. Katika mechi 4 za mwanzo tu walipata ushindi mara moja, vichapo viwili na sare moja. Sio mwanzo mzuri kwa timu kubwa inayosaka makombe.
Kiukweli 2024 ulikuwa mwaka mbaya. Lakini tangu kuanza kwa mwaka huu Wydad hawajapoteza mechi 4 mfululizo za ligi, wakifunga magoli 8, huku wao wakiruhusu mawili tu.
Hapa ndio pa kuanzia kwa Sele kufanya yake. Ameingia kwenye tanuri la moto ndani ya Wydad, achague moja; AIVE au AUNGUE.
Got a Questions?
Find us on Socials or Contact us and we’ll get back to you as soon as possible.