Safari ya Vazquez ndani ya Real Madrid imefika mwisho

Lucas Vázquez anatarajiwa kuondoka Real Madrid mwishoni mwa msimu wa 2024/2025, baada ya klabu hiyo kuamua kutompa mkataba mpya. 

Mkataba wake wa sasa unamalizika Juni 2025, na hadi sasa hakuna mazungumzo ya kuongeza muda wake, jambo linaloashiria kuwa klabu imeamua kuachana naye.

Katika msimu huu, nafasi ya Vázquez katika kikosi cha kwanza imepungua, hasa kutokana na ushindani mkubwa katika nafasi ya beki wa kulia. 

Fede Valverde amekuwa akitumika mara kwa mara katika nafasi hiyo, na pia kuna uwezekano wa Real Madrid kumsajili Trent Alexander-Arnold, jambo linalozidi kupunguza nafasi ya Vázquez.

Kwa sasa, klabu kama Sevilla FC, RCD Espanyol, na Real Mallorca zimeonyesha nia ya kumsajili Vázquez kwa uhamisho huru msimu ujao. 

Sevilla inamwona kama chaguo bora kwa sababu ya uzoefu wake na uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali, wakati Espanyol, klabu aliyowahi kuchezea kabla ya kurejea Madrid, pia ina ndoto ya kumrudisha nyumbani.  

Lucas Vázquez amecheza mechi zaidi ya 350 akiwa na Real Madrid, akishinda mataji 23, ikiwa ni pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tano. Amejulikana kwa uaminifu wake, uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali, na mchango wake mkubwa kwa klabu kwa kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

Iwapo ataondoka, mechi ya mwisho ya LaLiga dhidi ya Real Sociedad inaweza kuwa fursa ya mashabiki wa Real Madrid kumuaga mchezaji huyu wa muda mrefu katika Uwanja wa Santiago Bernabéu.

 Kwa Mara ya kwanza Lucas Vázquez alivaa jezi ya Real Madrid mwaka 2015 ikiwa ni timu kubwa huku akiwa amewahi kuzitumikia Madrid B na C katika nyakati tofauti tofauti.