Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema inatambua kuwa afya bora ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alieleza hayo wakati akizindua kampeni ya Zanzibar Afya Week 2025 inayotarajiwa kufanyika Mei 4 hadi Mei 10 Zanzibar, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege.
Amesema ili kufikia maendeleo endelevu, ni muhimu kuwa na watu wenye afya njema, kwani afya bora huongeza uzalishaji, inasaidia jamii kuwa na nguvu kazi bora na huchangia katika kupunguza mzigo wa magonjwa kwenye jamii na serikali.
Amesema Zanzibar Afya Week 2025 inahusiana moja kwa moja na vipaumbele vya serikali vilivyobainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 na Mpango wa Mkakati wa Afya wa Zanzibar III.
Aidha, amebainisha kuwa hiyo ni fursa adhimu ya kuimarisha mfumo wa afya, kukuza ubunifu katika sekta ya tiba, na kuhamasisha utalii wa afya hapa Zanzibar.
Mapema, Mwenyekiti wa Kamati ya Zanzibar Afya Week 2025, Salim Kikeke, amesema jambo hilo ni moja ya mikakati ya viongozi wakuu wa nchi kufanya kazi na sekta binafsi ili kuleta matukio chanya katika sekta ya afya.
Amesema moja ya ndoto za Rais Mwinyi ni kuifanya Zanzibar kuwa na utalii wa afya, hivyo watahakikisha wanatumia nafasi hiyo kuitangaza Zanzibar kimataifa na kuwafikia wadau mbalimbali ili waweze kuwekeza katika sekta hiyo.
Leave a Reply