Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imezindua rasmi Vituo 23 vya Kukusanyia Maziwa vilivyojengwa na kuboreshwa kupitia Mradi Shirikishi wa Wasindikaji na Wazalishaji wa Maziwa Tanzania (TI3P).

Uzinduzi huo wa kitaifa umefanyika katika Kituo cha Kukusanyia Maziwa cha Nshamba (Nshamba MCC), Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera, ukiongozwa na Mhe. Balozi Dkt.Bashiru Ally Kakurwa (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Waziri amesema mradi wa TI3P umeleta mageuzi makubwa katika mnyororo wa thamani wa maziwa nchini kwa kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa maziwa na kupanua masoko kwa wafugaji wadogo, wa kati na wakubwa.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege, amesema hadi sasa mradi umewezesha mikopo ya zaidi Shilingi bilioni 4, ununuzi wa mitambo 3,254 yenye thamani ya bilioni 10.8, ufadhili wa viwanda 15 vya usindikaji kwa Shilingi bilioni 22 huku ruzuku fungamanifu ya bilioni 1.448 kutolewa kwa wafugaji na wasindikaji wa maziwa.
Uzinduzi wa vituo 23 vya kukusanyia maziwa kupitia mradi wa TI3P unaashiria hatua mpya katika mageuzi ya sekta ya maziwa nchini. Hatua hii inaweka msingi imara wa uchumi wa viwanda unaotegemea uzalishaji bora, thamani iliyoongezwa na ushiriki mpana wa wafugaji katika mnyororo wa thamani wa maziwa.












Leave a Reply