Serikali Ya Tanzania Yalijibu Bunge La Ulaya

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa tamko rasmi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujibu azimio la Bunge la Ulaya lililotolewa tarehe 8 Mei 2025 kuhusu masuala ya kisheria yanayoendelea nchini.

Katika tamko hilo, Tanzania imeweka wazi msimamo wake thabiti wa kulinda mamlaka ya kikatiba, uhuru wa mihimili ya dola, na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kujenga taifa la kidemokrasia, jumuishi, na lenye kuheshimu haki za binadamu.

Tanzania imeeleza kwa uwazi kuwa inatambua na kuheshimu uhusiano wake wa muda mrefu na Umoja wa Ulaya, lakini haikubaliani na njia inayotumiwa na baadhi ya wabunge wa Bunge hilo kutoa maamuzi kwa kutumia taarifa zisizo sahihi au zenye mrengo wa kisiasa pasipo kujadiliana na serikali kupitia njia rasmi za kidiplomasia.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa hatua hiyo ni ukiukwaji wa misingi ya heshima kwa mamlaka ya kitaifa na ni kinyume na miongozo ya kimataifa ya uhusiano baina ya nchi huru.