Serikali Yaendelea Kufungua Fursa Za Kibiashara Za Nje Na Ndani Ya Nchi

Maonesho ya Kimataifa ya Biashara yamekuwa fursa kubwa na kuwanufaisha zaidi wafanyabiashara na wananchi. Wafanyabiashara kutoka nje ya nchi wanapokuja Tanzania kutafuta fursa za kibiashara, huacha fedha za kigeni kwa watoa huduma mbalimbali kama hotelini, usafiri na wengine huajiri wenyeji.

Wafanyabiashara na Wawekezaji nchini hawanabudi kuendelea kuchangamkia fursa za ubia na uwekezaji katika sekta ya vifungashio. Eneo hilo lina mchango mkubwa katika kuongeza thamani na ushindani wa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wadogo na wa kati.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb) alipokuwa anafungua maonesho ya kimataifa ya kilimo, chakula, vifungashio na karatasi Januari 29, 2026 Jijini Dar es Salaam na yanafanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia leo na yanashirikisha mataifa 16.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri Kapinga amesema Serikali inaendelea kufungua milango ya biashara ndani na nje ya nchi kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa, wafanyabiashara na mtu mmojammoja.

Aidha, ameongeza kuwa tukio hilo ni jukwaa muhimu kwa wakulima, wafugaji na wajasiriamali kujifunza teknolojia za kisasa na kupanua masoko ya bidhaa zao. Amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi na kwenda kushiriki maonesho hayo.

Pia maonesho hayo yanajumuisha teknolojia za kisasa za usindikaji wa nafaka, mashine za kusaga, vifaa vya plastiki pamoja na vifungashio vya aina mbalimbali vinavyosaidia kuongeza thamani ya bidhaa, hasa kwa wajasiriamali wadogo na kati kwani bidhaa zao zinahitaji vifungashio vizuri na bora ili kukubalika katika masoko ya Kimataifa na kwingineko.

Hatahivyo,Waziri Kapinga amewahakikishia wageni wote kutoka mataifa mbalimbali kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) ili kuhakikisha fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana katika maonesho hayo zinatumika kikamilifu.

Kwa upande wake, mwandaaji wa maonesho hayo, Leonard Nyaki, amesema kuwa maonesho yamewakutanisha wawezeshaji 32 kutoka mataifa 16, huku ushiriki wa Watanzania ukiwa bado mdogo katika sekta za kilimo, ufugaji, nafaka, plastiki, uzalishaji wa makaratasi, tishu pamoja na vifungashio vinavyowasaidia wajasiriamali wadogo wadogo.