Serikali yaingilia Kati, Sakata la Mtoto Shauri

Serikali wilayani Uvinza Mkoani Kigoma imeahidi kushirikiana na wadau ili kumtafutia Shule itakayokidhi mahitaji ya mtoto Shauri John ambaye hivi karibuni habari zake zimesambaa kupitia mitandao ya kijamii akionesha kuwa na uhitaji wa kupata Elimu bora huku akimlalamikia mzazi wake kwa kumpatia jukumu la kuchunga mifugo badala ya kusoma.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinah Mathamani alipotembelea kijiji cha Kawibili anapoishi mtoto huyo kwa lengo la kutoa taarifa kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali kwa kushirikiana na wadau walioguswa na taarifa huzo ili kuhakikisha anapata Mazingira bora ya kujiendeleza kitaaluma.

Akiwa kijijini hapo, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa Rai kwa wazazi kuepuka kuwapa wanafunzi majukumu yanayowanyima fursa ya kuhudhuria shuleni na kushiriki vipindi vya darasani na kuchangia utoro hali inayowapunguzia fursa ya kupata Elimu bora.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amewashukuru wote waliofanikisha kuibuliwa kwa taarifa za mtoto huyo sambamba na kuwa na dhamira ya kumsaidia, huku akisisitiza zoezi ka upokeaji wa michango kwa sasa linaratibiwa na ofisi yake likisimamiwa na Mkurugenzi mtendaji wa Wilaya hiyo kwa kushirikiana na Katibu Tawala Wilaya.

Kwa upande wake Mtoto Shauri ameeleza kuwa dhamila na malengo yake ni kupata elimu bora ambayo itaweza kufanikisha yeye kuwa Mhandisi na hataki tena kusomea pale kijijini.

Ameongeza kuwa wapo watu wengi wanaomtaka kumchukua na kumsaidia kumuwezesha kwenye masomo yake ambapo amewashukuru wadau wote wenye nia njema juu ya maisha yake