Shujaa wa Liverpool katika mtihani mzito 

Na Kelvin Lyamuya

DAKIKA mbili tu zilitosha kufuta dhambi zote za Darwin Nunez ambazo ziliandikwa kwa kila aina ya wino na wale wajiitao Wanazi wa Anfield na Waabudu Falsafa za Bill Shankly wakati Liverpool wakishinda mabao 2-0 nyumbani kwa Brentford.

Wakati Nunez akifunga mabao hayo mawili, mashabiki wa klabu yake wakasahau changamoto ambazo Nunez amekuwa akiwapa kama mshambuliaji namba 9 mwenye makali dhaifu pindi timu hiyo inapohitaji kila aina ya msaada wake ndani ya 18.

Hadi sasa kwenye Ligi Kuu, Nunez ameifungia Liverpool mabao 4 na kuchangia pasi 2 za mabao lakini, katika mechi zaidi ya 10 hiyo sio takwimu ya kuridhisha kwa mshambuliaji wa timu inayowania kombe na ikumbukwe kwamba Liverpool walilipa Euro Milioni 80 kumsajili.

Hata hivyo, mashabiki wa Liverpool au wapinzani wao kwa sasa wana maneno machache ya kusema kutokana na kwamba hakuna timu ya kumzuia Arne Slot, Virgil Van Dijk, Trent Alexander-Arnold, Mo Salah kubeba kombe la ligi ifikapo May, 2025.

Ule ushindi wa juzi pale GTech Community Stadium sio tu kwamba umewapaisha zaidi kileleni hao Liverpool, pia ni ushindi uliorudisha heshima kwa Nunez ambaye kwa sasa wapo wanaosema jamaa ni garasa na wapo wanaoamini jamaa bado ana kauli ya kusema mbele ya mastraika wenzake akina Erling Haaland na Alexander Isak.

Historia inasema kwamba Soka la England limedumu katika levo za juu kwa sababu ya kuishi katika msingi wa matumizi makubwa ya nguvu, kasi na hekaheka za kila aina, sifa ambazo Bwana Nunez anazo. Lakini hapa nawapa ukweli mchungu, Liverpool haina uhitaji wa mchezaji wa aina hiyo.

Kwanini Liverpool haina uhitaji na Nunez wa fujo na matumizi makubwa ya nguvu? Kwa sababu Kocha wake, Arne Slot anajaribu kuitengeneza timu yenye ubora unaoakisi mbinu za kocha aliyemtangulia ambaye ni Jurgen Klopp, Pep Guardiola na mtaalam mwingine aliyeko Real Madrid, Mzee Carlo Ancelotti.

Kwa namna hii, kiukweli Arne Slot yuko hatarini kuchelewa kimafanikio iwapo Nunez ataendelea kutegemea mlango wa ‘Chaotic football’ kuliko kuutumia mlango muhimu zaidi ambao tayari ulishafunguka mbele ya upeo wa macho yake ambao ni uwezo wa kupiga mashuti makali (ubora muhimu sana huu kwa #9).

Siri ambayo imemfanya Mohammed Salah kuwa mfungaji bora Liverpool kwa misimu zaidi ya mitano ni mwendelezo mzuri wa kiwango, na ndio siri inayopaswa kufunguliwa kwa hawa akina Nunez. Kwamba sasa kesi ya Nunez na mafowadi wenzake (muondoe Diogo Jota) inakuwa na pande mbili; Mosi ni jukumu la benchi la ufundi kurekebisha mfumo wa timu na kutoa mianya kwa wengine kufunga mabao zaidi.

Au, Darwin Nunez aisake consistency ya kutikisa nyavu kwa nguvu kabla hajajikuta njiapanda ndani ya klabu ambayo imempa nafasi ya kutosha ya kuonesha uwezo wake ambao ameuonesha vyema katika mechi kadhaa na kuwa shujaa wa Liverpool.