Simba vs Yanga: Mgogoro wa Maandalizi, Simba Yatangaza Kususia Mechi. Klabu ya Simba SC imesema imesikitishwa na vitendo visivyo vya kiungwana vilivyofanyika kuelekea mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Yanga SC, ambapo ikiwa kama timu mgeni, imenyimwa haki yake ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi. Kutokana na hali hiyo, Simba imetangaza kutoshiriki mchezo huo.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa na Menejimenti ya Klabu hiyo, Simba imeeleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 17 (45) ya Kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, timu mgeni inapaswa kuruhusiwa kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi angalau mara moja kabla ya siku ya mchezo katika muda rasmi wa mchezo husika. Hata hivyo, licha ya kufika uwanjani kwa wakati, Simba ilizuiwa kwa makusudi kufanya mazoezi yake.
Mazingira ya Kuzuiwa kwa Simba Kufanya Mazoezi
Taarifa hiyo inafafanua kuwa baada ya kikosi cha Simba SC kufika uwanjani kwa mujibu wa ratiba, kilielezwa na Meneja wa Uwanja kuwa hana maelekezo ya kuruhusu mazoezi kufanyika bila kibali cha Kamishna wa Mchezo. Baada ya Kamishna wa mchezo kufika, hali bado haikubadilika, kwani walinzi wa Klabu ya Yanga (mabaunsa) walivamia msafara wa Simba na kuzuia kikosi hicho kuingia uwanjani kwa ajili ya mazoezi huku wakifanya vurugu.
Simba inasema kuwa licha ya jitihada zake za kutafuta suluhisho kwa zaidi ya masaa mawili, bado haikuweza kufanya mazoezi, hali iliyosababisha kuondoka eneo la uwanja kwa sababu za kiusalama. Tukio hilo limeandikwa rasmi na ushahidi wake kurekodiwa kwa hatua zaidi.
Simba Yatangaza Kutocheza Mchezo Huo – Yanga Waendelea na Maandalizi
Kufuatia ukiukwaji huu wa taratibu za mchezo, Simba SC imetangaza rasmi kuwa haitoshiriki mechi hiyo na inahifadhi haki zote za kisheria juu ya uamuzi huo. Klabu hiyo pia imetoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika wa tukio hilo ili kuhakikisha haki inatendeka na vitendo vya aina hii havijirudii katika michezo mingine ya ligi.

Hata hivyo, kwa wakati huohuo, watani wao wa jadi Yanga SC wameonesha nia ya kuendelea na maandalizi kwa ajili ya mchezo huo unaopangwa kuchezwa saa 1:15 usiku. Swali linabaki, jee, Simba watakubali kupeleka timu yao uwanjani ama watabaki na msimamo wao wa kutoshiriki mchezo huo?
Mashabiki wa soka nchini wanabaki kusubiri kuona mustakabali wa mchezo huu mkubwa wa watani wa jadi, huku macho yakielekezwa kwa hatua ambazo TFF na Simba itachukua dhidi ya tukio hili.
Leave a Reply