Simba yafuzu Nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC), Rais Samia awapongeza

Klabu ya Simba Sports Club imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF Confederation Cup), baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 4-1 dhidi ya Al Masry ya Misri, mchezo uliopigwa leo Aprili 9, 2025 katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam

Katika michezo ya nyumbani na ugenini, kila timu ilishinda kwa mabao 2-0 nyumbani kwake, hivyo kuifanya jumla ya mabao kuwa sare ya 2-2. Hali hiyo ilisababisha mshindi wa jumla kupatikana kwa njia ya mikwaju ya penalti, ambapo mlinda mlango wa Simba SC, Moussa Camara, aliibuka shujaa kwa kuokoa mikwaju miwili ya wapinzani na kuiwezesha timu yake kusonga mbele.

Huu ni ushindi wa kihistoria kwa Simba SC, Mafanikio haya yanadhihirisha ukuaji wa kiwango cha klabu hiyo na mchango wake katika kuiwakilisha vyema Tanzania katika ramani ya soka la Afrika.

Kutokana na mafanikio hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa pongezi rasmi kwa klabu hiyo akisema:

“Pongezi za dhati kwa Klabu ya Simba kwa ushindi katika mchezo wa mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup). Ushindi wenu ni furaha kwa mashabiki wenu na burudani kwa Watanzania wote. Ninawatakia kila la kheri katika hatua ya Nusu Fainali.”


Uongozi wa Simba SC pia umewashukuru mashabiki, benchi la ufundi, wachezaji na wadau wote waliotoa mchango wao katika kuhakikisha timu inapata mafanikio hayo. Klabu hiyo inaendelea na maandalizi kuelekea mchezo wa nusu fainali kwa lengo la kufikia fainali na kutwaa taji la CAFCC.