TAA, TCAA, ATCL na TMA zasaini makubaliano ya ankara jumuishi

Dar es Salaam, Tanzania – Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), na Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) leo zimetia saini makubaliano muhimu ya utekelezaji wa Ankara Jumuishi, ikiwa ni hatua ya kihistoria katika kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizo katika sekta ya usafiri wa anga.

Makubaliano hayo yamesainiwa na viongozi wakuu wa taasisi husika: Bw. Abdul Mombokaleo (TAA), Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Daniel Malanga, Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Chang’a, na Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Mhandisi Peter Ulanga.

Lengo kuu la makubaliano haya ni kuweka mfumo wa pamoja wa Ankara utakaorahisisha michakato ya malipo kati ya taasisi hizi nne, huku ukilenga kuongeza uwazi, ufanisi, na uwajibikaji katika utendaji wa kila siku. Mpango huu pia unatarajiwa kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja na wadau wa sekta ya anga kwa ujumla.
Wakuu wa taasisi hizo wametoa shukrani kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAA Bw. Abdul Mombokaleo kwa kuwa kinara wa wazo hili na kwa kujitolea kwake kwa moyo wote kuhakikisha linatimia, na kutoa wazo la namna ya utekelezaji.

Pamoja na hayo hatua hii ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe; Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo amesisitiza umuhimu wa taasisi za umma kushirikiana kwa karibu kupitia mifumo inayosomana ili kuongeza tija, kupunguza urasimu, na kuboresha huduma kwa wananchi.

Kupitia makubaliano haya, taasisi hizo zinatarajia kuimarisha mahusiano ya kimkakati, kubadilishana taarifa kwa wakati, na kushirikiana kwa ufanisi katika kuhakikisha ukuaji endelevu wa sekta ya usafiri wa anga nchini.