Taasisi za wizara ya Viwanda na Biashara zatakiwa kuchochea uanzishaji wa viwanda nchini

Wizara ya Viwanda na Biashara ni moja ya muhimili mkuu katika ustawi wa uchumi wa Tanzania, ambapo kupitia taasisi zake 13, inabeba jukumu la msingi la kuchochea uanzishaji na uendelezaji wa sekta ya viwanda na biashara, kuzalisha ajira, kuongeza pato la Taifa na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Katika kuhakikisha dhamira hiyo inatimia, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Waziri Salum, ametoa agizo madhubuti kwa Wakuu wa Taasisi hizo kuondoa urasimu na kuwa wawezeshaji wa sekta binafsi, hatua inayolenga kuifanya nchi kuwa na uchumi shindani wa viwanda unaoendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum, Februari 21, 2026, jijini Arusha wakati akifungua kikao kazi cheke na Wakuu wa Taasisi (zikiwemo NDC, TEMDO, CAMARTEC, TIRDO, SIDO, TBS, BRELA, FCC, WMA, WRRB, FCT, TANTRADE, na CBE). Kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kujadili mikakati ya taasisi hizo katika kutekeleza majukumu yao na kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza na Wakuu hao, amesema Wizara inategemewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuchochea uanzishwaji wa viwanda na biashara kwa kasi na kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha kuongeza ajira, kukuza pato la Taifa na kujenga uchumi shindani wa Viwanda.

Vilevile, amesisitiza taasisi hizo kutangaza shughuli na huduma wanazozitoa ili kuwawezesha wananchi kuzifahamu na kuzitumia katika kukuza biashara na uanzishwaji wa viwanda vitakavyoleta tija kitaifa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Aristides Mbwasi, amewasisitiza wakuu hao wa taasisi kuhakikisha wanaondoa changamoto mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.

Naye, Mwenyekiti wa Wakuu wa Taasisi na Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Prof. Mkumbukwa Mtambo, pamoja na Wakuu wengine wa Taasisi wamemhakikishia Katibu Mkuu kuwa wako tayari kutekeleza maelekezo hayo na kuahidi kuwa wawezeshaji wakuu kwa wafanyabiashara na kuondoa vikwazo vinavyojitokeza.