Tanzania na Angola kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kidiplomasia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongeza
juhudi za Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço kudumisha
uhusiano na urafiki wa muda mrefu baina ya nchi hizi mbili na kuwa makubaliano
yaliyofikiwa kwenye ziara yake nchini Angola yataenda kuimarisha uhusiano wa
kiuchumi.

“Kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi katika nchi zetu mbili, ikiwemo kwenye sekta za
Kilimo, Utalii, Viwanda na Uchumi wa Buluu, tumekubaliana kuimarisha mahusiano ya
biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu, Ni kwa msingi huo, tumeshuhudia utiaji saini
wa Hati ya Makubaliano ya ushirikiano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na
Angola Private Investment and Export Promotion Agency (AIPEX), ikiwa ni hatua
muhimı ya kukuza kiwango cha uwekezaji baina ya nchi mbili hizi,” amesema Rais Dkt.
Samia.

Rais Dkt. Samia ametoa pongezi hizo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari
kwenye mkutano wa pamoja na mwenyeji wake Mhe. Rais João Manuel Gonçalves
Lourenço katika Ikulu ya nchi hiyo iliyopo Luanda.

Aidha, katika kumarisha zaidi ushirikiano uliopo baina ya watu wa Tanzania na Angola na
kuzidi kukuza biashara na uwekezaji, Rais Dkt, Samia ametangaza kuwa Tanzania pia
itaondoa sharti la kulipia visa ya utalii kwa raia wa Angola kuingia Tanzania, kama
ambavyo Serikali ya Jamhuri ya Angola ilivyoondoa sharti hilo kwa raia wa Tanzania
kuingia nchini humo tangu mwaka jana

Kwa upande wake, pamoja na mambo mengine, Rais Lourenço ameridhia mwaliko wa Rais
Dkt. Samia kufanya ziara nchini Tanzania mwezi Julai, 2026 ambapo mbali ya ziara hiyo
atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kihistoria wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya
Biashara Dar es Salaam, yatakayoambatana na mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania
na Angola

Vilevile, leo Rais Dkt Samia na mwenyeji wake Rais Lourenço wameshuhudia utiaj
saini wa Mikataba ya ushirikiano katika masuala ya ulinzi pamoja na Hati ya makubaliano
kuhusu kukuza Uwekezaji.

Awali, Rais Dkt. Samia alianza ziara yake kwa kutembelea Mnara wa Kumbukumbu katika
Makumbusho ya António Agostinho Neto, Muasisi na Rais
Wa Kwanza Wa Angola, ambapo aliweka shada la maua na kutoa heshima katika kaburi la muasisi huyo

Katika hatua nyingine, kufuatia mwaliko wa Mhe. Carolina Cerqueira, Spika wa Bunge lo
Jamhuri ya Angola, Rais Dkt. Samia amelihutubia Bunge hilo, ambapo pamoja na mambo
mengine amesema kuwa nchi za Afrika zinatakiwa kupambana katika vita ya uchumi kwa
moyo uleule ambao waasisi wa mataifa ya Angola na Tanzania walivyopambana
kuzikomboa nchi zao kutoka kwenye ukoloni

Aidha, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Tanzania na Angola zimekubaliana kuunganisha
nguvu katika kuongeza fursa za kiuchumi kwa watu wa nchi hizi, hususan vijana. Katika
kuimarisha mahusiano haya, Rais Dkt. Samia ametangaza kwamba Serikali ya Jamhuri ye
Muungano wa Tanzania inakusudia kufungua upya Ubalozi wake nchini Angola