Tanzania Yathibitisha Visa Viwili vya Ugonjwa wa Mpox

Dar es Salaam, Machi 10, 2025 – Wizara ya Afya imethibitisha uwepo wa visa viwili vya ugonjwa wa Mpox nchini baada ya uchunguzi wa maabara kuthibitisha maambukizi hayo mnamo Machi 9, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara, wagonjwa hao walihisiwa kuwa na dalili za vipele usoni, mikononi, miguuni na sehemu nyingine za mwili, pamoja na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, na maumivu ya viungo. Mmoja wa wahisiwa ni dereva wa magari ya mizigo aliyesafiri kutoka nchi jirani kuelekea Dar es Salaam.

Baada ya kupokea taarifa hizo mnamo Machi 7, 2025, sampuli zilichukuliwa na kupelekwa katika Maabara ya Taifa kwa uchunguzi. Matokeo yalithibitisha kuwa watu wawili wameambukizwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox.

Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na vituo vya kutolea huduma za afya, inaendelea na juhudi za ufuatiliaji na utambuzi ili kubaini wahisiwa wengine na kuwapatia huduma stahiki.

Mpox ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyotokana na wanyama jamii ya nyani. Binadamu anaweza kuambukizwa kupitia kugusana na wanyama wenye maambukizi au mtu mwingine aliyeambukizwa.

Serikali imeeleza kuwa inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika mipaka ya nchi, upimaji wa wasafiri wanaoingia na kutoka, pamoja na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu hatua za kujikinga na ugonjwa huu.

Kwa kuwa magonjwa mengi yanayosababishwa na virusi hayana tiba maalum, Wizara ya Afya inawasihi wananchi kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi.