Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua mwezi wa Elimu na Kutatua Changamoto za Walipakodi ili kuendelea kuwahudumia kwa karibu zaidi Walipakodi katika maeneo yao na kutatua changamoto za kikodi zinazowakabili.
Akifanya uzinduzi huo Juni 06.2025 Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema lengo la kampeni hiyo ya kutoa Elimu na kutatua changamoto za Walipakodi ni kutaka kuwafikia Walipakodi wengi zaidi katika maeneo yao.
“Desemba 2024 tulikuwa na kampeni ya Shukrani kwa Mlipakodi ambayo tuliendelea nayo mpaka Januari 2025 ambayo ilitufikisha katika makundi mbalimbali ya Walipakodi na kuwasikiliza ndiyo maana tumeona ni vema tunapokwenda kufunga mwaka wa fedha tuzindue Elimu na kutatua changamoto za Kodi kwa Walipakodi” Mwenda
Amesema lengo la kauli mbiu hiyo ya Juni ni kuendeleza ushirikiano na Walipakodi na kuhakikisha wanawafikia wote katika maeneo yao huku akisisitiza kipaumbele cha TRA kikubwa kuwa ni kurahisisha biashara nchini.
Amesema kauli mbiu hiyo imekuja wakati muafaka TRA ikiwa imeongeza idadi kubwa ya Watumishi wapya 1896 ambao watapelekwa katika kila Kona ya Tanzania kwa lengo la kutatua changamoto za Kodi na kutoa Elimu kwa Mlipakodi.
Amebainisha kuwa ni matarajio ya Serikali kwamba waajiriwa hao wataleta mabadiliko ya kiutendaji TRA kwa kuongeza wigo wa Kodi na idadi ya Walipakodi ambao wengi wao hawajafikiwa Bado.
Ametoa wito kwa Watumishi hao wapya kujiepusha na vitendo vya Rushwa na uvunjifu wa maadili na badala yake watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma.
Leave a Reply