Trump Asitisha Misaada ya Kijeshi kwa Ukraine

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesitisha misaada yote ya kijeshi kwa Ukraine kufuatia mvutano wake na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, wiki iliyopita, afisa wa Ikulu ya White House amethibitisha.

“Rais Trump amekuwa wazi kuwa anataka amani. Tunataka pia washirika wetu wajitolee kwa lengo hilo. Tunasitisha misaada yetu na kuikagua ili kuhakikisha inachangia katika suluhu,” alisema afisa huyo siku ya Jumatatu, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Ikulu ya White House haijatoa maelezo kuhusu aina na kiasi cha misaada kitakachosimamishwa wala muda wa hatua hiyo. Pentagon pia haijatoa taarifa zaidi kuhusu suala hilo.

Haya yanakuja baada ya mabishano makali kati ya Trump na Zelenskiy katika Ikulu ya White House siku ya Ijumaa ambapo Trump alimtuhumu kwa kutoshukuru vya kutosha kwa uungaji mkono wa Washington katika vita na Urusi.