Tundu Lissu na Othman Masoud Wazuiliwa Kuingia Angola

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, pamoja na viongozi wa ACT Wazalendo wakiongozwa na Kiongozi wa Chama, Ndugu Dorothy Semu, na Mwenyekiti wa Chama, Ndugu Othman Masoud Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar wanadaiwa kuzuiliwa kuingia nchini Angola walipokuwa wakielekea kushiriki mkutano wa Jukwaa la Demokrasia Afrika (The Platform for African Democrats – PAD)

Taarifa kutoka kwa ACT Wazalendo na CHADEMA zinaeleza kuwa viongozi hao walizuiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Luanda, ambapo hati zao za kusafiria zilichukuliwa na mamlaka za Serikali ya Angola bila maelezo yoyote, Serikali ya Angola imeagiza viongozi hao warejeshwe Tanzania.

Mkutano huo, uliopangwa kufanyika tarehe 13-16 Machi 2025, umeandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation na ulikuwa unatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya viongozi 40 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

Katika hatua ya kulaani kitendo hicho, ACT Wazalendo wameitaka Serikali ya Angola kutoa maelezo ya sababu za kuzuiliwa kwa viongozi hao na kurudisha hati zao za kusafiria. Aidha, vyama hivyo vimetoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania kumuita Balozi wa Angola nchini ili atoe maelezo juu ya tukio hilo.