Mgombea Urais aahidi Kumwachia huru Lissu endapo atashinda Uchaguzi Mkuu

NIKIWA RAIS NAMUACHIA HURU TUNDU LISSU, ATENGENEZE KATIBA MPYA – GOMBO

Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Mhe. Gombo Samandito Gombo, ameahidi kumuachia huru mwanasiasa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, endapo atashinda uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza leo Septemba 4, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika mkoani Shinyanga, Gombo amesema taifa la Tanzania haliwezi kuwa na amani ya kweli bila haki kutendeka kwa kila mmoja, amesisitiza kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha Tundu Lissu anaachiwa huru pamoja na kuunda kamati maalum ya kutengeneza katiba mpya.

Vipaumbele vingine alivyovitaja ni pamoja na kufuta kikokotoo cha mafao ya wafanyakazi, kutoa huduma za afya bure, kufuta mikopo ya elimu ya juu na kutoa msamaha wa madeni ya wanafunzi waliokopeshwa na serikali, ili kila Mtanzania awe na nafasi ya kupata elimu.

Kwa upande wake, mgombea mwenza wa urais kupitia CUF, Husna Mohammed, amesema rasilimali zilizopo mkoani Shinyanga hazilingani na hali halisi ya maisha ya wananchi, hivyo amewasihi wakazi wa mkoa huo kufanya uamuzi sahihi siku ya uchaguzi ili kuleta mabadiliko ya kweli.

✍🏼: @officialkimoco
#WasafiDigital