Serikali imepongezwa kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika bandari mbalimbali hapa nchini hususani bandari ya Dar es Salaam ambayo sasa imekuwa na ufanisi mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara ya kikazi bandarini jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dkt Joseph Mhagama amesema upanuzi na uboreshaji wa bandari hiyo imekuwa lulu kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
“Leo tumekuja kwenye ziara yetu ya kawaida ya kikazi iliyo na lengo la kujionea utekelezaji wa miradi ya uboreshaji na upanuzi wa bandari hii ya Dar es Salaam”, alisema Dkt Mhagama.
Dkt Mhagama aliongeza kuwa taarifa ya uwekezaji huo haipo kwenye makaratasi tu bali ipo kwa vitendo, ndio maana mapato ya bandari yameongezeka na idadi ya wateja imeongezeka pia.
“Kwa hakika uwekezaji wa bandari hii umeifanya Bandari hii kuwa ni kitovu cha Utalii nchini, kwani mpaka hivi sasa kwenye mapato ya TRA yanaonesha bandari hii imechangia kwa asilimia 30”, alisisitiza Dkt Mhagama.

Aidha, Dkt Mhagama alisema kuwa wao kama kamati inayohusiana na masuala ya sheria mbalimbali, watashirikiana na TPA pamoja na Wizara ili kuhakikisha changamoto za kisheria zinatatuliwa ili kuongeza ufanisi kwa mamlaka hiyo kwani wameambiwa muingiliano wa kisheria ni mojawapo ya changamoto wanayokumbana nayo.
“Pamoja na hayo yote, kwa niaba ya Kamati hii ambayo mimi ninaiongoza tunampongeza Rais Samia kwa uthubutu na uwekezaji mkubwa anaoufanya kwenye miradi mbalimbali ya kimkakati sio tu hapa bali miradi yote hapa nchini”, alihitimisha Dkt Mhagama.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Bw. David Kihenzile akimuwakilisha Waziri wa Wizara hiyo Profesa Makame Mbarawa alisema kuwa wamepokea taarifa hiyo ya Kamati ya Bunge na kuahidi kuifanyia kazi.
“Nipende kuipongeza kamati hii, kwani mara zote imekuwa na maono kama aliyonayo Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan ya kutaka bandari zetu ziwe zinachangia pato kubwa katika nchi”, alisema Bw Kihenzile.
Leave a Reply