Uhamiaji kuwasaka matapeli wa nafasi za ajira

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji imetoa tahadhari juu ya uwepo wa matapeli, wanaolaghai wananchi kupitia mitandao ya kijamii kwa njia ya sms, ya kuwa kuna nafasi za ajira, na kuwataka wananchi kutuma fedha ili kusaidiwa kupata nafasi hizo.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Aprili 2, 2025 na Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Paul Mselle imeeleza kuwa utapeli huo umeibuka hivi karibuni, kufuatia idara hiyo kutoa tangazo la kuitwa kwenye mafunzo ya uhamiaji kwa vijana wa kitanzania kupitia tovuti na mitandao yake ya kijamii, lakini mchakato huo ulishakamilika, na uliendeshwa na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za ajira, hivyo wananchi wanaombwa kupuuza, na watoe taarifa pindi wanapopigiwa simu au kutumiwa ujumbe.

Aidha, idara hiyo inaendelea na uchunguzi kwa lengo la kuwabaini wanaohusika na uhalifu huo, ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.