Uhamiaji yakanusha uwepo wa kituo cha Polisi kinachohudumia raia wa China waishio nchini

Idara ya Uhamiaji imekanusha vikali taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwepo kwa kituo cha polisi kinachoitwa Chinese Overseas Service Center katika maeneo ya Victoria, jijini Dar es Salaam, kinachodaiwa kutoa huduma za kipolisi kwa raia wa China wanaoishi nchini.

Kupitia taarifa rasmi, Idara hiyo imeeleza kuwa baada ya kufanya uchunguzi wa kina, imebainika kuwa kituo kinachodaiwa kuwa cha polisi ni ofisi halali ya jumuiya iitwayo Chinese Overseas Service Centre, iliyoko Mtaa wa Makumbusho, Kata ya Kijitonyama, Wilaya ya Kinondoni – Barabara ya Old Bagamoyo. Jumuiya hiyo ni tawi la China Business Chamber of Tanzania.

Kwa mujibu wa Uhamiaji, jumuiya hiyo imesajiliwa kisheria na kazi yake ni kutoa msaada wa kijamii na kiutawala kwa raia wa China walioko Tanzania, sawa na jinsi jumuiya za raia wa mataifa mengine zinavyofanya huduma kama hizo nchini. Aidha, taasisi hiyo siyo kituo cha Polisi, kama ilivyodaiwa kwenye video iliyoenea mitandaoni.

Uhamiaji imeeleza kuwa taarifa hizo zinalenga kupotosha umma na kuchochea taharuki isiyo ya lazima. Hivyo, imetoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa hizo na kuendelea kuwa watulivu huku vyombo husika vikiendelea kufuatilia mienendo ya taasisi zote zinazofanya kazi ndani ya nchi kwa mujibu wa sheria.