Utata Kifo cha Mtoto Janeth, Baba Afunguka

Mtoto wa miaka 8 mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Tumsiime iliyopo Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera Janneth Mbegeya amefariki dunia huku kifo cha mtoto huyu kikigubikwa na utata hali inayopelekea familia ya mtoto huyo kukosa imani na matokeo ya uchunguzi wa madaktari.

Akiongea kwa majonzi na masikitiko makubwa nyumbani kwake baba wa Marehemu Janeth Asimwe Mbegeya Enock Mbegeya amesema awali daktari katika hospitali teule ya Rubya aliwaeleza kuwa mtoto wao amefanyiwa vitendo vya ukatili wa kubakwa na kulawitiwa na kisha kuchomwa sindano inayosadikika kuwa ya sumu.

Baba huyo ameendelea kueleza kuwa baada ya muda mfupi daktari aliyewapa taarifa hiyo alikana kauli hiyo na kusema kuwa mtoto huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi mengine.

Katika hatua nyingine baba huyo ameiomba serikali kufanyia kazi uchunguzi huo ili mwanaye aweze kupata haki yake.

Akithibitisha tukio hilo kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera Kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi Blasius Chatanda amesema kuwa mtoto huyo baada ya kufanyiwa vipimo aligundulika alikuwa anasumbuliwa na upungufu wa damu, maji Pamoja na njaa kali licha ya kuwa wazazi hawakukubaliana na majawabu hayo.