Vyama 18 vya siasa vyenye usajili kamili, Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wamesaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 leo tarehe 12 Aprili, 2025 jijini Dodoma.
Vyama hivyo ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), Civic United Front (CUF), National Convention for Construction and Reform (NCCR), Union for Multiparty Democracy (UMD), National League for Democracy (NLD), United Peoples’ Democratic Party (UPDP) na National Reconstruction Alliance (NRA), African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA).
Vyama vingine ni Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP), Madini Kilimo Nishati (MAKINI), Democratic Party (DP), Sauti ya Umma (SAU), Alliance for African Farmers Party (AAFP), Chama cha Kijamii (CCK), Alliance for Democratic Change (ADC) na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) na Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo).
Kwa upande wa Serikali Kanuni hizo za maadili zilisainiwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi na kwa upande wa Tume alisaini Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele.
Awali akizungumza kabla ya utiaji saini, Jaji. Mwambegele alivishukuru vyama vya siasa kwa ushirikiano wao wakati wote wa uandaaji wa kanuni hizo za maadili.
“Tunawashukuru viongozi wote wa Vyama vya Siasa kwa namna ambavyo mmekuwa mkiipa ushirikiano Tume katika utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali hususan yale yanayohusu mchakato wa maandalizi ya uchaguzi, ikiwemo uandaaji wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi ambazo tupo hapa leo kwa ajili ya kutia saini kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025,” alisema Jaji Mwambegele.
Amesema Tume imeandaa kanuni hizo za maadili ambazo zitatambulika kama Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025 kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya Mwaka 2024.
Leave a Reply