Muungano wa makundi ya waasi, wakiwemo waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, umetangaza usitishaji wa mapigano kuanzia leo Jumanne kwa sababu za kibinadamu.
Kwa Mujibu wa BBC, muungano huo ulieleza kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza mateso ya raia waliokumbwa na mapigano makali katika siku za hivi karibuni. Waasi hao wamesema hawana nia ya kupanua maeneo wanayoyashikilia, ingawa awali walikuwa wametangaza azma ya kuendelea na mashambulizi.
Umoja wa Mataifa Umezema takriban watu 900 wameuawa na wengine 2,880 wamejeruhiwa katika mapigano yanayoendelea katika na karibu na mji wa Goma, mji mkubwa mashariki mwa DRC.
Hali hiyo imesababisha maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limeripoti kuwa zaidi ya watu 400,000 wamelazimika kuyahama makazi yao tangu mwanzoni mwa mwaka 2025.
Mataifa ya G7 na Umoja wa Ulaya (EU) yamelaani mashambulio hayo, yakiyataja kuwa ukiukaji wa wazi wa uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hali ya usalama mashariki mwa DRC inazidi kuzorota, huku jumuiya ya kimataifa ikihimiza juhudi za kidiplomasia ili kupata suluhisho la kudumu kwa mzozo huu.
Leave a Reply