Wafugaji wawapiga wakulima, walisha mazao yao Nachingwea

Wakulima wa Kijiji cha Lionja B, Kata ya Lionja, Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, wamelalamikia vitendo vya ukatili vinavyodaiwa kufanywa na wafugaji wahamiaji, ikiwa ni pamoja na kupigwa na kuharibiwa kwa mazao yao kutokana na mifugo kulishwa mashambani.

Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, wananchi hao walisema kuwa hali hiyo imekuwa chanzo cha kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji, na kuhatarisha amani kijijini humo.

Aidha, wananchi walitoa shutuma dhidi ya baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi kwa madai ya kutokuwa waadilifu na kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wafugaji wanaokiuka sheria.

Akijibu malalamiko hayo, Kaimu Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nachingwea (OCD), SP Jereneus Nguruwe, alieleza kuwa jeshi hilo limepokea malalamiko na tayari limeanza kuyafanyia kazi ili kuhakikisha mgogoro huo unapatiwa suluhu ya kudumu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, alikiri kuwapo kwa changamoto za nidhamu miongoni mwa baadhi ya askari wa jeshi la polisi na kumtaka OCD kuchukua hatua za kuwaonya askari wake.

Moyo aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali na vyombo vya dola katika kutatua mgogoro huo kwa njia ya amani na maelewano.