Wanafunzi wawili wa shule ya Blessing Modern iliyopo Mtaa wa Nyasaka, wilayani Ilemela, Mkoa wa Mwanza, waliotekwa Februari 05, 2025, wamepatikana wakiwa salama, huku watuhumiwa wa utekaji wakiuawa katika majibizano ya silaha na polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, amesema kuwa wanafunzi hao walikuwa wamefichwa ndani ya nyumba namba 8, iliyopo Mtaa wa Nyabulogoya, Kata ya Nyegezi, jijini Mwanza.
Katika operesheni ya kuwaokoa, polisi walikumbana na upinzani kutoka kwa watuhumiwa hao, hali iliyosababisha majibizano ya silaha kati ya pande hizo mbili. “Watuhumiwa walijaribu kupambana na askari kwa kutumia silaha, lakini kwa juhudi za jeshi la polisi, waliwadhibiti na wanafunzi waliokolewa wakiwa salama,” alisema Kamanda Mutafungwa.
Hadi sasa, haijafahamika sababu halisi ya utekaji huo, huku vyombo vya usalama vikiendelea na uchunguzi zaidi kubaini iwapo ulikuwa na nia ya kutaka fidia au sababu nyinginezo.
Leave a Reply