Wasanii waaswa kusajili kazi zao na majina yao ya kisanii

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Suleimani Jaffo, ametoa wito kwa Wasanii kusajili majina yao ya kisanii BRELA kama alama ya biashara na kazi zao COSOTA kwa ajili ya kuweka ulinzi.

Waziri Jaffo ametoa wito huo alipokuwa akifungua mkutano wa maadhimisho ya Miliki Ubunifu Duniani Kitaifa yaliyofanyika leo Mei 21, 2025 Dar es Salaam, yenye Kauli Mbiu isemayo Muziki na Miliki Bunifu: Sikiliza Mdundo wa Miliki Bunifu.” yaliyoratibiwa na BRELA kwa kushirikiana na COSOTA.

“Napenda kuwapongeza Wasanii wote wa Muziki waliosajili majina yao BRELA akiwemo Diamond Platinum, Nandy, Zuchu, Mrisho Mpoto na wengine wote, usajili huu unatoa nafasi kubwa ya kukuza kipato na kufanya biashara kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.
Akiendelea kuzungumza Mheshimiwa Waziri huyo alisema hapo nyuma Wasanii wengi wamepoteza haki zao ijapokuwa wamefanya kazi kubwa kwa sababu hawakuzingatia haya.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa amesema licha ya Muziki wa Tanzania kuvuka mipaka ya nchi, Wasanii wengi bado hawajachukua hatua ya kusajili kazi zao, jambo linalowanyima fursa ya kunufaika na kazi hizo kisheria.

“Tunasisitiza Muziki si burudani tu, ni biashara na biashara yoyote inalindwa kisheria, hivyo Wasanii wengi wamekuwa wakipoteza mapato kwa sababu kazi zao hazijasajiliwa,” alisema Nyaisa.