Washindi wa Tuzo za Wachekeshaji: Tanzania Comedy Awards 2025

Tuzo za kwanza za Tanzania Comedy Awards zimefanyika Februari 22, 2025, katika ukumbi wa The Super Dome Masaki, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kama mgeni rasmi. Hafla hiyo iliwakutanisha wachekeshaji maarufu nchini, ikiwa ni jukwaa la kutambua na kuthamini mchango wao katika sekta ya vichekesho.

Katika tuzo hizo, mchekeshaji chipukizi Dogo Sele alifungua dimba kwa kushinda kipengele cha ‘Best Funny Kid’, akithibitisha kipaji chake cha uchekeshaji tangu akiwa mdogo.

Aidha, Coy Mzungu, mwanzilishi wa jukwaa la vichekesho ‘Cheka Tu’, alitunukiwa Tuzo Maalumu ya ‘Game Changer’ kwa mchango wake mkubwa katika kuleta mapinduzi kwenye tasnia ya vichekesho nchini. Tuzo hiyo ilitangazwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, kama ishara ya kuthamini juhudi zake katika kuwapa fursa wasanii wa vichekesho kupitia jukwaa lake la Cheka Tu.



Kwa upande wa Mchekeshaji Bora Maalum wa Mwaka, Jol Master aliibuka mshindi, licha ya kushindwa kuhudhuria hafla hiyo kutokana na matatizo ya afya. Katika kipengele hicho, alishindana na wachekeshaji wengine wakali akiwemo Kipotoshi, Deo Matius, na Nalim Noseph.

Mchekeshaji mkongwe Lucas Mhavile ‘Joti’ aling’ara kwa kushinda tuzo mbili: ‘Best Comedian Actor of the Year’ na ‘Best Legend People’s Choice of The Year’. Katika tuzo yake ya pili, Joti alichuana na wachekeshaji wakongwe akiwemo Bambo, Asha Boko, Maufundi, Mukwele, Kigwedu, Senga, Muhogo Mchungu, na Brother K.



Kwa upande wa wanawake, Asma Jamida aliibuka mshindi wa tuzo ya Mchekeshaji Bora wa Kike, huku Nanga akishinda tuzo ya Mchekeshaji Bora wa Kiume wa Mwaka. Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said, katika hafla hiyo.



Katika kipengele cha Shoo Bora ya Runinga, kipindi cha ‘Kitim Tim’ kilijizolea tuzo, kikizishinda shoo nyingine maarufu kama Futuhi, Original Comedy, na Mbambalive.

Kwa upande wa wachekeshaji wa ucheshi wa kusimama (stand-up comedy), Neila Manga aliibuka mshindi wa ‘Best Female Stand-Up Comedian of the Year’, akiwashinda Mambise na Mama Mawigi. Wakati huohuo, Mc Eliud, maarufu kama Mr. Sukari, alitwaa tuzo ya ‘Best Stand-Up Comedian’ kwa upande wa wanaume, akiwashinda Leornado, Kipotoshi, na Deo Rashid.



Katika kipengele cha Mchekeshaji Bora wa Kidijitali, Mama Mawigi aliibuka mshindi kwa upande wa wanawake, huku TX Dulla akishinda tuzo hiyo kwa upande wa wanaume, akiwashinda Steve, Ndaro, na Nanga.



Tuzo ya ‘Best Comedy Duo of the Year’ ilikwenda kwa Ndaro na Steve Mweusi, ambao walitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda Nanga na Shafii, pamoja na Zuli Comedy.

Kwa upande wa uigizaji wa vichekesho, Safina wa Mizengwe alishinda tuzo ya Mwigizaji Bora wa Vichekesho wa Kike, akiweka rekodi katika tasnia hiyo.

Mchekeshaji Leonard Datus (maarufu kama Leonardo) ameshinda kwenye  kipengele cha Mchekeshaji bora wa Jumla kwa Wanaume na wanawake.



Katika hafla hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alipewa tuzo ya ‘Champion of Comedy’, kama ishara ya kutambua mchango wake katika kuunga mkono sekta ya vichekesho nchini Tanzania.



Kwa ujumla, Tanzania Comedy Awards 2025 imeonyesha ukuaji wa tasnia ya vichekesho nchini, kwa kutambua na kuthamini juhudi za wachekeshaji mbalimbali katika kuburudisha na kuelimisha jamii kupitia sanaa ya uchekeshaji

Zifuatazo ni Picha za Matukio mbalimbali kwenye hafla ya utoaji wa Tuzo za Wasanii wa Komedi Tanzania (TCA) iliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Februari, 2025.