Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Steven Wasira, amesema kuwa sababu kuu iliyosababisha kuundwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 ilikuwa ni kuhakikisha usalama na kudumisha amani ya kudumu kati ya mataifa hayo mawili.
Akizungumza mbele ya mamia ya wakazi wa Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma, katika maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano huo, Wasira alieleza kuwa viongozi wa wakati huo walitambua umuhimu wa mshikamano ili kuzuia hatari ya migogoro ya ndani na vitisho vya kigeni.

“Muungano huu ulilenga kujenga ngome imara ya amani, kulinda Mapinduzi ya Zanzibar, na kuhakikisha kuwa wananchi wa pande zote mbili wanaishi kwa mshikamano, uhuru, na usalama wa kudumu,” alisema Wasira huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria.
Aliongeza kuwa kupitia Muungano, taifa limefanikiwa kuondoa mizizi ya udini na ukabila ambayo ingeweza kuvuruga mshikamano wa kitaifa.
“Leo hii, Mtanzania anatambulika kwa utaifa wake na sio dini wala kabila lake. Haya ni mafanikio makubwa ya Muungano wetu wa kihistoria,” alisisitiza Wasira.
Alibainisha kuwa miaka 61 ya Muungano imeleta mafanikio makubwa katika nyanja za uchumi, elimu, afya, na miundombinu, huku akisisitiza kuwa umoja uliopo leo ni matokeo ya maamuzi ya busara yaliyofanywa na waasisi wa Muungano huo.

“Leo tunaadhimisha sio tu miaka 61 ya historia, bali miaka 61 ya amani, upendo, mshikamano wa kidini na kikabila, na maendeleo yaliyopatikana kwa sababu ya Muungano huu wa kipekee,” aliongeza.
Katika hotuba yake, Wasira pia aliwahimiza wananchi wa Chemba kuendelea kuuenzi Muungano kwa kuimarisha mshikamano na kuendeleza jitihada za maendeleo katika maeneo yao.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia na viongozi wa serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chemba.
Leave a Reply