Watatu wahukumiwa kunyongwa hadi kufa Geita

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Geita imewatia hatiani na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa watuhumiwa watatu kati ya wanne katika Kesi ya Mauaji Na. 29820 ya mwaka 2024 iliyoanza kusikilizwa Januari 07, 2025.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Thereza Luhedeka (73) (dada wa marehemu), Mateso Joseph (23) (mtoto wa Thereza Luhedeka) na Elias Galawa (49) (mganga wa kienyeji) wote wamepatikana na hatia ya kula njama na kushiriki kumuua Joyce Luhedeka (51), Msukuma, Mkazi wa Ikobe, Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita. Mbali na hukumu hiyo, Mahakama imemwachia huru Dogan Budeba (44).

Wakili wa Serikali Liberatus Rwabuhanga akiwa na wakili Ipyana Mwantonto na Scholastica Tiffe wameieleza Mahakama kuwa, Oktoba 11, 2023 washtakiwa walimuua Joyce Luhedeka akiwa nyumbani kwake kwa kumkata na kitu chenye makali sehemu mbalimbali za mwili wake, kosa ambalo ni kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, (Sura ya 16, rejeo la mwaka 2022).

Baada ya kumuua, walizikata sehemu za siri na kutoweka nazo hadi walipokamatwa na kukutwa wakiwa wamezikausha. Uchunguzi ulibaini sehemu hizo za siri ni za marehemu Joyce Luhedeka, pia chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina.

Akisoma hukumu hiyo Machi 28, 2025, Mhe. Fredrick R. Lukuna, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, amesema Mahakama imezingatia kwa makini na tahadhari kubwa katika kufikia uamuzi huo baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka ambapo mashahidi 16 waliitwa na kutoa ushahidi pamoja na ule wa utetezi na kujiridhisha pasipo kuacha shaka yoyote; washtakiwa watatu walitenda kosa la kumuua Joyce Luhedeka na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa ili iwe fundisho kwa watu wengine.