Watu Wanne Waokolewa Kwenye Mgodi Shinyanga, Mmoja Afariki Hospitalini

Vigil light, candle with the miner belongings (helmet, gloves, pickaxe, vest, belt) after the fatal accident in the mine

Idadi ya watu waliookolewa wakiwa hai kwenye ajali ya mgodi wa wachimbaji wadogo wa dhahabu wa Wachapakazi Gold Mine uliopo kijiji cha Nyandolwa, Wilaya ya Shinyanga imeongezeka na kufikia wanne, hadi sasa, bado watu 21 hawajapatikana tangu mgodi huo utitie na kuwafukia watu 25.

Mmoja kati ya watu wa nne aliyeokolewa jana mchana majira ya saa sita, alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini kwa matibabu. Tukio hilo limezidisha simanzi kwa familia na wananchi waliokusanyika nje ya mgodi wakisubiri taarifa za wapendwa wao waliokwama chini ya ardhi.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amesema juhudi za uokoaji zinaendelea kwa ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama, wachimbaji wa kujitolea pamoja na taasisi mbalimbali na kutaja majina ya watu waliokwishaokolewa huku akiwahakikishia wananchi kuwa serikali inafanya kila jitihada kuwaokoa wengine.

Baadhi ya ndugu wa watu waliofukiwa kwenye mgodi huo wameiomba serikali kuongeza juhudi na vifaa katika zoezi la uokoaji kwa ndugu na jamaa zao waliokwama ardhini.

Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Stephen Kiruswa, amefika eneo hilo na kutoa maelekezo kwa viongozi wa mkoa na wilaya kuhakikisha kuwa hatua stahiki zinachukuliwa haraka na kusisitiza umuhimu wa usalama wa wachimbaji wadogo na kueleza kuwa serikali itafanya tathmini ya kina kuhusu mazingira ya migodi ya aina hiyo.