Watuhumiwa sita wakamatwa kwa tuhuma za mauaji Arusha


Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia watuhumiwa 06 kwa tuhuma za mauaji ya mtu mmoja aitwaye Wilson Mbise (25) mkazi wa King’ori, wilaya ya Arumeru mkoani humo ambaye alifariki dunia baada ya kujeruhiwa sehemu mbambali za mwili wake.

Akitoa taarifa hiyo leo Agosti 15, 2025, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Salvas Makweli amesema mtu huyo alifariki dunia Agosti 11, 2025 huko katika msitu wa Mazingira uliopo katika Kijiji cha Muungano, kata ya King’ori wilayani Arumeru baada ya kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake. 

ACP Makweli amebainisha kuwa watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa  pamoja na kutekeleza tukio hilo la mauaji pia waliwajeruhi watu wengine wanne sehemu mbalimbali za miili yao kwa tuhuma za wizi na wanaendelea kupatiwa matibabu.

Amewataja majeruhia hao kuwa ni Daud William (17), Kelvin Humphrey (22), Godbless Emmanuel (30) na Allen Nanyaro (21) wote ni wakazi wa kata ya King’ori, Wilaya ya Arumeru na wanaendelea na matibabu.

Aidha amesema kuwa wanaendelea kukamilisha upelelezi wa tukio hilo na pindi utakapokamilika taratibu nyingine za kisheria zitafuata huku akibainisha kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mount Meru Arusha kwa uchunguzi wa Daktari.

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limewaonya baadhi ya watu wanaojichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha mila kuacha mara moja tabia hiyo, badala yake pindi wanapowakamata watuhumiwa watoe taarifa kwa vyombo husika ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.