Kufuatia Tanzania kupata fursa na heshima ya kuwa nchi mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati (Africa Energy Summit) utakaofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 27 – 28 Januari, 2025, Serikali imeelekeza kuwa siku hizi mbili watumishi wa umma katika Mkoa wa Dar es Salaam wafanyie kazi nyumbani, ili kuepuka usumbufu ambao unaweza kusababishwa na kufungwa kwa baadhi ya Barabara kufuatia Ugeni huu Mkubwa.
Taarifa iliyotolewa kwa umma na Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Kusiluka imewataka watumishi wa umma katika Mkoa wa Dar es Salaam wafanyie kazi nyumbani isipokuwa wale ambao mazingira yao ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vya kazi kama vile watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya na sekta ya usafiri na usafirishaji.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Benki hazitafungwa na biashara katika Soko la Kariakoo zitaendelea kufanyika. Hoteli na migahawa nayo haitafungwa.
Aidha, Waajiri katika sekta binafsi wameshauriwa kuruhusu watumishi wao katika Mkoa wa Dar es Salaam kufanyia kazi nyumbani au kuweka utaratibu ambao hautasababisha changamoto ya usafiri kutokana na kufungwa kwa barabara hizo.
Leave a Reply