Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amewataka Wananchi kulinda miundombinu ya Anwani za Makazi, akisema kuwa Serikali imepata taarifa kwamba vibao vya Anwani za Makazi, vinavyoonesha mitaa na barabara, vinaondolewa na watu wasio waaminifu na kisha kuuzwa.
Mhe. Majaliwa aliyasema hayo leo, Februari 8, 2025, katika hafla ya Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi, iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC).
“Tunazo taarifa kwamba, Anwani za Makazi tulizoziandika kwenye nyumba zetu, vibao tulivyoviweka kuonesha mitaa na barabara Watanzania wasio waaminifu, wanang’oa na kwenda kuviuza. Watanzania, Serikali yetu imetumia gharama kubwa kutengeneza mifumo hii na kuweka kwenye mitaa yetu, ni muhimu kwetu kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii,” alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa aliielekeza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha kwamba maandalizi ya Sheria ya Anwani za Makazi yanaendelea na kuwawezesha wananchi kutumia Anwani za Makazi wakati wa kutoa na kupokea huduma, hususan huduma zinazohitaji kutambulisha Anwani za Makazi.

Aliongeza kuwa, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inapaswa kufanya maadhimisho haya kuwa endelevu na kuwa na hadhi ya kimataifa kwa kuwakaribisha nchi nyingine kushiriki.
Alisisitiza pia umuhimu wa Wizara kushirikiana na wadau wengine ili kutoa vishikwambi kwa watendaji wa kata, mitaa, vijiji na shehia, ili kurahisisha utendaji kazi katika ngazi hizo.

Waziri Mkuu Majaliwa ameielekeza Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kusimamia utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi katika ngazi za Mikoa na Halmashauri, ikiwa ni pamoja na kuteua waratibu wa mfumo huo na kuwapa mafunzo ya uratibu.
Kwa upande wa Wizara ya Fedha, Mhe. Majaliwa ameitaka kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuboresha Mfumo wa NaPA kwa kuongeza moduli mpya itakayohusiana na vyombo vya moto. Vilevile, Wizara za Uchukuzi, Ujenzi, na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari zishirikiane kuhakikisha kuwa magari ya Serikali yanafungwa mfumo wa NaPA na kuhamasisha watoa huduma za usafirishaji kutoka sekta binafsi kufunga mfumo huo ili kurahisisha utambuzi wa maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), alieleza kwamba Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI, imejipanga kuhakikisha mfumo wa Anwani za Makazi unakuwa endelevu.
“Tutaendelea kufanya uhakiki wa taarifa, kujenga uwezo kwa watendaji wetu wa Serikali za Mitaa ili waendelee kuhuisha taarifa; kutunga Sheria ya Anwani za Makazi, kuboresha Mfumo wa kidijitali wa NaPA na kuhamasisha matumizi ya Anwani za Makazi,” alisema Waziri Silaa.

Leave a Reply