WHO yaipongeza Tanzania kwa hatua za Kudhibiti Changamoto za Afya



Tarehe 16 Januari 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Ghebreyesus, akiwa ameandamana na wataalamu wa afya kutoka mataifa mbalimbali, alizungumza na vyombo vya habari kwa njia ya mtandao kupitia Zoom, YouTube, na LinkedIn. Katika kikao hicho, alitoa muhtasari wa masuala ya afya duniani na kugusia hali ya afya katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania. 

Kuhusu Tanzania, Dkt. Tedros alibainisha kuwa WHO imepokea taarifa za haraka za hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto za afya mkoani Kagera. Serikali imepeleka timu ya taifa ya dharura (National Response Team), maabara zinazotembea, pamoja na vitengo vya matibabu kwa ajili ya kushughulikia hali hiyo. 

WHO imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi hizo na imesisitiza utayari wake wa kutoa msaada wowote unaohitajika ili kuhakikisha changamoto hiyo inakabiliwa kikamilifu. 

Aidha, Dkt. Tedros ameishauri Serikali ya Tanzania kuhakikisha sampuli zilizokusanywa mkoani Kagera zinapelekwa kwenye maabara za rejea za kimataifa kwa uchunguzi wa kina, pamoja na kukusanya sampuli za ziada kwa kuzingatia taratibu za kawaida za afya ya umma. 

Pia, ameipendekeza Serikali kuimarisha ufuatiliaji wa washukiwa wa ugonjwa husika kwenye mipaka ya mkoa huo, sambamba na kushirikiana na nchi jirani ili kuongeza uwezo wa kubaini na kutibu washukiwa wa ugonjwa huo. 

Kwa kumalizia, Dkt. Tedros alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na juhudi za pamoja katika kuhakikisha masuala ya afya yanashughulikiwa kwa ufanisi duniani kote.