Klabu ya Young Africans SC imejibu taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inayodai klabu hiyo ina deni, huku Yanga ikisisitiza kuwa haijawahi kulipwa fedha zake za ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa misimu mitatu mfululizo.
Katika taarifa yake, Yanga imesema haijalipwa fedha za ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa misimu ya 2021/2022, 2022/2023, na 2023/2024. Klabu hiyo imedai kuwa TFF imekuwa ikishikilia fedha hizi kwenye akaunti zao kila msimu unapomalizika, licha ya kufahamu kuwa ni makosa na kinyume cha utaratibu.
“Hakuna uthibitisho wowote wa kimaandishi kuonyesha kama TFF wamewahi kulipa fedha hizi za Ubingwa kwa Klabu ya Yanga,” imesema taarifa hiyo, ikiongeza kuwa ni “aibu na fedheha na kumtia dosari mdhamini kuendesha mashindano bila kumlipa Bingwa kwa misimu mitatu mfululizo.

Yanga imesisitiza kuwa dawa ya deni ni kulipa kwa wakati, kwani hiyo ni haki ya mshindi na inampa heshima mdhamini wa mashindano. Imefafanua kuwa ada za malipo ya wachezaji wa kigeni ambazo TFF imezitaja hulipwa mwanzoni mwa msimu mpya, huku fedha za ubingwa hutolewa mwisho wa msimu.
Klabu hiyo pia imebainisha kuwa haijawahi kupokea taarifa yoyote rasmi kutoka TFF kuhusu klabu yao kuwa na deni kwa shirikisho hilo.
Uongozi wa Young Africans unaendelea kusisitiza kulipwa pesa zao za ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB kwa msimu wa 2023/24, ili waweze kucheza mchezo wa fainali utakaofanyika tarehe 28 Juni, 2025.
Leave a Reply