Zitto Kabwe achukua fomu kugombea Ubunge Kigoma Mjini

Kiongozi mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amechukua rasmi fomu ya kuwania ubunge wa jimbo la Kigoma Mjini.


Zitto Kabwe, ambaye amekuwa mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika eneo hilo, alikabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa Jimbo la Kigoma Mjini, Idd Adam, katika hafla fupi iliyohudhuriwa na wafuasi wake.


Kwa mujibu wa Taarifa ya Zitto Kabwe, Jana jioni wana kwaya kutoka Kanisa la Moravian Kigoma walimfanyia maombi rasmi na leo asubuhi alizuru kwenye makaburi ya Rubengela alipozikwa Mama yake Mzazi Hajjat Shida Salum na baadae Zawiya za kinamama katika Mji wa Kigoma Mjini walimfanyia Dua maalumu.

Aidha Saa Tano asubuhi Wanawake zaidi ya 600 kutoka Matawi yote 72 ya ACT wazalendo Kigoma mjini walitembea nae Kilomita mbili kutoka Ofisi ya ACT Wazalendo Mkoa, Rubuga Ujiji mpaka Ofisi za Jimbo Buzebazeba.

“Ilikuwa ni shughuli ya Wanawake wa Mji kwa heshima ya mwenzao ‘Da Shida’. Ninaukabidhi mchakato mzima wa mimi kurejea Bungeni kwa Wanawake wa Mji wa Kigoma Ujiji. TUTASHINDA KWA KUPAMBANA!”- amesema Zitto ambaye aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa Vipindi viwili.