Kwanini tunatakiwa kuzingatia ubora wa miguu yote kuanzia timu ya vijana?

Katika mchezo wa soka, iwe ni kocha au mchambuzi na wakati mwingine hata watangazaji wa Radio na TV wote hawa wanaweza kuwa na mtazamo sawa juu ya umuhimu wa timu kuwa na mchezaji mwenye uwezo wa kutumia miguu yote iwe ni kutoa pasi, kupokonya mpira au kujaribu bahati golini.

Huo ni utajiri mkubwa sana kwa mchezaji. Sifa chache tu anazoweza kuwa nazo mchezaji wa aina hii ni pamoja na; 

Ufundi wa kutumikia nafasi tofauti katika mfumo. 

Miondoko au mipango yake uwanjani huwa haitabiriki kirahisi.

Ana mzani sawa kiumbile na kubwa zaidi akiipiga pasi yake ni lazima iwe imenyooka na inafika kwa mlengwa.

Mchezaji mwenye ubora wa namna hiyo hujitambulisha kama mburudishaji kwa wale wenye kiu ya soka maridhawa na kiukweli, wapo wengi tu ambao wameiburudisha dunia kwa utaalamu wao wa kupiga chenga na guu la kulia halafu anaweka nyavuni na la kushoto.

Miaka ya nyuma Zinedine Zidane alifanya yote kwa ufasaha akitumia miguu yake miwili. 

Aliificha na kulia kabla ya kuihamishia kushoto. Alipoifichua mali akaitoa na kulia halafu akaipokea tena na kushoto. 

Kazi ya kumtabiri fundi huyu ikawa ngumu kwa sababu alichokifanya kilikuwa ni nje ya mipango ya wapinzani.

Historia pia inamkumbuka beki nguli wa AC Milan na timu ya Taifa Italia, kipaji halisi Paolo Maldini. Huyu ndiye yule beki makini, akili nyingi na hakuwa mchoyo wa ‘moments’ za kuhadithia vizazi vijavyo ndani ya miaka 25 pale San Siro.

Sasa Milan ambayo aliitumikia Maldini enzi hizo ilikuwa inacheza kwenye ligi bora yenye mkusanyiko wa mastaa wakubwa ila bado mtihani ukawa mzito kupita kwa mwamba huyo. 

Ronaldo De Lima anaifahamu vyema kazi ya Maldini. Fundi Ronaldinho Gaucho naye ni shahidi wa uimara wa Maldini. 

Na wote walishawahi kukiri hadharani kwamba Maldini alikuwa jiwe haswa! Yaani mtu chuma aliyeweza kufanya ‘tackling’, kupiga pasi sahihi na yote aliyoweza kuyafanya kwa kutumia miguu yote miwili huku akicheza beki ya kushoto.

Hadi hapa ulipofikia pengine unajiuliza huyu mwandishi ana lengo gani dhidi ya wanaotumia mguu mmoja? 

Kwamba kwa aina ya wachezaji, mfano Diego Maradona wa Argentina au John Bocco wa Azam na Simba, ambao mguu mmoja ndio ulikuwa na nguvu zaidi ndio waonekane hawana umuhimu dhidi ya mafundi wa miguu yote?

Binafsi naamini hakuna mwenye umuhimu kumzidi mwingine, kilicho muhimu ni kuwaunganisha katika mfumo thabiti halafu matokeo yake lazima yawe bora, ni lazima timu iwe na mzani sawa katika msingi huu. 

Anayetumia mguu mmoja + anayetumia miguu yote wana madhara makubwa wakiunganisha nguvu. Huo ndio msingi wa makala hii.

Sasa, kwanini kichwa cha habari kinasisitiza umuhimu wa kuzingatia utafutaji wa wachezaji hawa na pia uboreshaji wa matumizi ya miguu yote kwa wale waliopo timu za vijana? Kwa sababu naamini hakuna klabu ya soka iliyo na malengo mazuri na mpira wetu hapa nchini halafu isiwe na maskauti.

Na hao maskauti kazi zao zinajulikana, kwa faida tu ya wasomaji ni kwamba kocha anapoamini mbinu zake zitasaidia kuwaongezea wachezaji ubora wa matumizi ya miguu yote basi lazima skauti awe sawa na mawazo ya aina hiyo na hapo ndipo jukumu la utafutaji linapoanzia kwake.

Kocha yeyote wa hapa nyumbani akitazama marejeo ya picha mjongeo za fundi Santiago Cazorla (Arsenal), winga hatari Ousmane Dembele (PSG) au mtaalamu kutoka Msumbiji, Jose Luis Miquissone (Simba) halafu akatumia mifano hiyo kuwanoa vijana kwa kipindi kirefu, basi lazima matokeo yapatikane.

Kwa mujibu wa tafiti iliyofanyika mwaka 2009; ‘The Returns to Scarce Talent: Footedness and Player Remuneration in European Soccer’ iliyoandikwa na Alex Bryson (University College London, England) na Bernd Frick (Paderborn University, Ujerumani),

Tafiti inaeleza kwamba “…matumizi ya miguu yote huanza kuonekana kwa mchezaji mwenyewe lakini, ni uwezo unaohitaji maboresho kwa kiasi kikubwa na kwa kupitia mazoezi.

“Hata hivyo, mazoezi hayo ni lazima yafuate ngazi za ukuaji wa mchezaji na haitawezekana tena kupandikiza ubora wa ziada katika matumizi ya miguu yote ikiwa mchezaji ameshautumia muda wake mwingi katika soka la ngazi za juu…” mwisho wa kunukuu.

Nitakupa mfano, Stephanie Aziz Ki huwa anaonekana mzembe anapolazimisha kutumia mguu wa kushoto kwenye eneo ambalo wengi huamini anaweza akatumia wa kulia, lakini ndio haiwezekani hata kama benchi la ufundi linajitahidi kuboresha hilo.

Ingawa tayari mguu wake wa kushoto ndio wenye nguvu zaidi na ndio wenye faida kwa Yanga.

Sasa swali ni je, huko katika timu zao za vijana wanafanya jitihada zipi kuwanoa katika suala la matumizi ya miguu yote ili kuweka mahesabu sawa na wale wenye faida kubwa licha ya kutumia mguu mmoja?

Kuna changamoto ambazo hawa maskauti huwa wanakutana nayo na nimeona sio mbaya kuiweka hapa ili isionekane kama hawaifanyi kazi yao vizuri.

Skauti anaweza kuwa katika majukumu ya kutazama vijana wenye umri kati ya miaka 10 na 12 ambao pia wanakuwa wanafuatiliwa na klabu tofauti kutoka duniani kote na katika zoezi zima la uchunguzi na uchambuzi, baadhi ya vijana hao wanaweza kuwapiku wengine na kuziweka klabu njiapanda.

Hapo sasa kuna uwezekano mkubwa vijana watano hadi sita (wanaotumia mguu mmoja) wakaibuka kuwa bora zaidi ya wawili ambao wanatumia miguu yote. 

Kazi ya skauti inaongezeka mara mbili kwa maana ni lazima aweke mahesabu sawa kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho na uamuzi huo ukikosa majina hayo mawili ya ‘walioshindwa’ basi, uwezo wa skauti utakuwa ni wenye mashaka. 

Na kama asipoondoka na hayo majina mawili linaibuka swali jingine, kwamba kocha aliyemuagiza kufanya ufuatiliaji huo pia nae huenda akawa na uwezo mdogo wa kuboresha vipaji? 

Kwa maana kijana ameshaonesha ana uwezo wa kutumia miguu yote, kwa umri wake mdogo akionekana huo uwezo wake haufai katika baadhi ya mifumo au maeneo ya uwanja, si ana muda wa kutosha wa kufundishwa zaidi? Kwanini asisajiliwe?

Sidhani kama ni sahihi kwa skauti au kocha kuwa na kikomo cha ugunduzi wa vipaji pamoja na utatuzi wa changamoto za ukuaji wa vijana kisoka. Maana yake ni nini? Hii itasababisha tukose kuwaona akina Miquissone au Zidane wa miaka ijayo.

Asilimia zaidi ya 50 ya wanasoka wote duniani ni watumiaji wa mguu mmoja, hasa mguu wa kulia. Na ndio maana ni nadra kupata mafundi wa miguu yote. Lakini maskauti nao hawatakiwi kufanya uchambuzi wao wa kiskauti kwa kuweka vikomo vya matumizi ya vijana wenye ubora huu adimu.

Ni lazima hapa kwetu tuliweke hili suala katika vipengele vya juu kabisa pindi klabu zinapotuma maskauti kusaka vipaji.

IMEANDALIWA NA KELVIN LYAMUYA