Rais Samia asema 4R zisiwe Kisingizio cha Kuvunja sheria, Ahutubia Taifa

π‘¨π’”π’Šπ’”π’Šπ’•π’Šπ’›π’‚ π’–π’Žπ’–π’‰π’Šπ’Žπ’– π’˜π’‚ π’Œπ’–π’…π’–π’Žπ’Šπ’”π’‰π’‚ π‘΄π’–π’–π’π’ˆπ’‚π’π’ π’˜π’‚ π‘»π’‚π’π’ˆπ’‚π’π’šπ’Šπ’Œπ’‚ 𝒏𝒂 π’π’‚π’π’›π’Šπ’ƒπ’‚π’“ π’Œπ’˜π’‚ π’Œπ’–π’…π’–π’Žπ’Šπ’”π’‰π’‚ π‘¨π’Žπ’‚π’π’Š 𝒏𝒂 π‘΄π’”π’‰π’Šπ’Œπ’‚π’Žπ’‚π’π’

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia falsafa yake ya 4R, utekelezaji wa falsafa hiyo lazima uende sambamba na kuheshimu Katiba na sheria za nchi.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo wakati akilihutubia Taifa leo Ijumaa usiku tarehe 25 Aprili 2025.

Ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais Dkt. Samia amesema falsafa ya R-4 itaendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza demokrasia na ushiriki wa wananchi katika masuala ya msingi ya Taifa.

Hata hivyo, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa kamwe falsafa hiyo ya 4-R haiwezi kutumika kama kisingizio cha kuvuruga amani au utulivu wa nchi.

β€œDemokrasia yetu imeendelea kukua na kuimarika, hususani kupitia falsafa yetu ya R-4 ambayo itaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kukuza ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi kwenye masuala muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu,”

β€œHata hivyo, ninataka kusisitiza kama ambavyo nimekuwa nikisema katika majukwaa mbalimbali kwamba kutekelezwa kwa falsafa ya R-4 kunaendana sambamba na kuzingatiwa kwa Katiba na sheria za nchi. Kamwe falsafa hii haiwezi kuwa kisingizio cha kuvunja sheria au kuvuruga mazingira yanayohatarisha amani, usalama na utulivu wa nchi yetu”

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo wakati ambapo Taifa letu la Tanzania linaelekea katika maadhimisho ya Muungano wa kihistoria kati ya Tanganyika na Zanzibar, yaliyoasisiwa Aprili 26, 1964.

Vilevile, Rais Dkt. Samia amesisitiza umuhimu wa kulinda mafanikio ya Muungano kwa kudumisha mshikamano, amani na umoja miongoni mwa Watanzania wa pande zote mbili za Muungano