BIMA za afya kwa wasanii wa Tanzania kuanzishwa

Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bwana Hamis Mwinjuma (mwanafa) leo ameongoza kikao kazi maalum kilicholenga kujadili na kuandaa msingi wa kuanzisha bima za afya kwa wasanii wa Tanzania. Kikao hicho kimejumuisha viongozi wa taasisi za sanaa, mashirikisho, na wadau mbalimbali wa sekta ya sanaa, likiwa na lengo la kuhakikisha wasanii wanapata ulinzi wa kiafya kwa ajili ya maisha ya sasa na baadaye.

Kwa kaulimbiu ya “SANAA BIMA: Ishi Sasa na Baadaye,” mpango huu unalenga kuwahamasisha wasanii kujiunga na mifumo ya bima inayowapa fursa ya kupata huduma bora za afya, kuimarisha uzalishaji wa kazi za sanaa kwa kuwa na afya bora, na kuwahakikishia usalama wa maisha yao kwa siku zijazo.

Katika kikao hicho, mtaalamu Eberhard Osward aliwasilisha mawazo na mapendekezo ya kitaalamu kuhusu namna bora ya kutekeleza mpango wa bima za afya kwa wasanii. Wazo hili linatarajiwa kuwa suluhisho muhimu kwa changamoto za kiafya zinazowakabili wasanii wengi, huku likiwa sehemu ya jitihada za serikali kuboresha ustawi wa sekta ya sanaa na maisha ya wadau wake.