Na Kelvin Lyamuya
WAKATI ule ambapo Simba Sports Club inakubali kuwaaga Wazambia, Clatous Chama na Rally Bwalya na hapohapo ikatangaza ujio wa Peter Banda na Pape Ousmane Sakho, kila mtu aliamini soka letu sasa linaishi katika uhuru wa kweli.
Miaka michache baadae tukagundua kumbe uhuru huo ulikuwa ni ndoto. Vijana wakaondoka wakiwa bado wadogo na kama haitoshi, ile ‘potential’ waliyokuja nayo ikawafuata hukohuko walikoenda, sisi wakituachia tafakuri zisizo na muafaka.
Tafakuri hizo ndio tunazo hadi leo kwa hawa akina Elie Mpanzu Kibisawala. Tunawaza, hapa tumepigwa? Au ndio tumeachwa kusubiri tena miaka na miaka hadi pale tutakaposhuhudia picha sawasawa na tunayoiona kwa mtoto wa msela wa Morocco, Lamine Yamal ama Estevao Messinho kutoka mitaa ya Brazil.

Tunapojiuliza kuhusu uhalali wa Elie Mpanzu kutambulika kama picha mpya ya burudani na mafanikio ya muda mrefu ndani ya Simba, tuyakumbuke na maamuzi (ya kibinafsi) ya kutosimamia kwa weledi na umakini maendeleo ya vijana mabarobaro kama The Wonderkid Peter Banda na mfungaji wa moja ya mabao bora zaidi Afrika, Pape Sakho maarufu P.O.S.
Baada ya kukupa historia ya bahati ya mtende iliyowapita Simba Sports Club kwa hawa vijana wawili mithili ya msichana mrembo anayempita kando kabisa kijana mchovu wa pochi na mwenye domo zito, sasa ngoja niwape Wanasimba uhalisia ambao wanapaswa kuishi nao kwa huyu Mpanzu Kibisawala.
Kuna ‘makosa’ yaliyofanyika kwa vipaji vya Banda na Sakho na hayapaswi kabisa kurudiwa kwa Elie Mpanzu. Kwa maana, kama kipaji hiki kutoka DR Congo ndicho kilichoivutia taasisi kongwe ya soka ambayo ni Simba, basi mipango ya kiufundi izingatiwe ili mchezaji huyu asiwe tu na faida kwa klabu, pia Ligi Kuu inahitaji sura ya matangazo huko duniani na miguu ya Kibisawala imedhihirisha kuwa na uwezo huo.
Sina uhakika kama Elie Mpanzu atadumu Tanzania kwa zaidi ya miaka 5. Maana tumekuwa na desturi ya kuchoka kula pilau na kutamani tembele kitu ambacho sio dhambi, ila kwa wanaojua biashara ya soka, huyu Kibisawala ni ‘icon’ ya vipaji halisi na maridhawa kama Bernard Morison ama Iddy Nado.
Katika upande muhimu, Simba wanatakiwa kuwa serious mno na maendeleo ya Elie Mpanzu ambaye ninaamini kwa weledi wake lazima atajisimamia kwanza yeye ili kuboresha palipopungua ingawa najua wapo wanaoamini jamaa ni nyongeza bora zaidi katika kikosi cha Simba.
Ana nguvu ya kusukuma mashambulizi muda wote (energetic) na ndio sifa kuu ya mchezaji mbunifu. Hii inatupeleka kwenye hitimisho dogo la kwamba, kwa sasa Jean-Charles Ahoua ni kama anautua mzigo mzito wa kufanya kazi zote za ubunifu ndani ya uwanja. Huu ni ushindi mwingine kwa Simba katika eneo la usajili.
Sidhani kama kuna mtu atashindwa kunielewa nikisema kwamba ninamuonea sana wivu kocha Fadlu Davids kwa jinsi kazi yake inavyobebwa vyema na watu wanaofahamu mahitaji halisi ya kiufundi ndani ya timu. Na hali hiyo inamsaidia hata yeye kung’amua mbinu safi za kuishi na wachezaji wenye vipaji maridhawa kama Elie Mpanzu Kibisawala.
“I’m very happy with Mpanzu, how he’s adapted, how he’s come into the team. We can see the threat is there. The goals will come. He has so many attacking skills within his arsenal. So, it’s just a matter of time. And when he does start scoring, I’m afraid he won’t stop,” Fadlu Davids.
Naam, Fadlu Davids amepata mchezaji sahihi wa kushirikiana na kikosi chenye nyota kadhaa wenye ufundi mkubwa wa soka, ukiirudia kusoma comment yake hapo juu kuhusu Elie Mpanzu, utagundua hilo.
Fadlu ana furaha na hata motisha pia huwa zinakuja zenyewe bila kutumia nguvu.
Sasa, isitokee tena mtu akavuruga hii chemistry iliyopatikana baina ya mkufunzi mkuu na wachezaji hawa ambao Simba wamewapata, la sivyo majuto yatakuwa makubwa kuliko ilivyotokea kwa Sakho na Banda ambao nadiriki kusema kwamba walikuwa na uwezo mkubwa na muda wa kutosha wa kuisafisha kabisa taswira nzima ya Simba Sports Club ambayo inautafuta tena ufalme wake.
Got a Questions?
Find us on Socials or Contact us and we’ll get back to you as soon as possible.