Kocha aliyeinoa Man United ateuliwa kuinoa Harambee Stars

Mamlaka za soka nchini Kenya zimetangaza kumteua aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa West Ham, Celta Vigo, Ajax na mmoja kati ya makocha wa Manchester United, Benni McCarthy, kuwa kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa hilo kufuatia mazungumzo yaliyodumu tangu December, 2024.

Mwaka 2023 McCarthy aliteuliwa na aliyekuwa Kocha Mkuu wa United Eric Ten Hag kuwa mmoja kati wa makocha wa mbinu katika kikosi cha Man United.

McCarthy atashirikiana na wasaidizi wake, kocha wa zamani wa klabu ya Richards Bay, Vasili Manousakis sambamba na golikipa wa zamani wa Afrika Kusini na Orland Pirates, Moeneeb Josephs.

Benchi hilo jipya la ufundi litaanza majukumu yake mara moja kuelekea mitanange miwili muhimu ya kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia ambapo Harambee Stars watakuwa na kibarua cha ugenini dhidi ya Gambia kabla ya kuwavaa Gabon katika uwanja wa nyumbani, wiki chache zijazo.