CCM Yaweka Ukomo wa Vipindi Viwili kwa Viti Maalum Wanawake

Dodoma, 11 Machi 2025 – Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Taifa imefanya kikao maalum tarehe 10 Machi 2025, jijini Dodoma, chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika kikao hicho, Halmashauri Kuu ilipokea na kujadili agenda kuu mbili ambazo ni Mapendekezo ya Marekebisho ya Kanuni za Uteuzi wa Wagombea Uongozi katika Vyombo vya Dola toleo la 2022 na Rasimu ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 – 2030.

Marekebisho ya Kanuni za Uteuzi

CCM imefanya mabadiliko muhimu katika Kanuni za Uteuzi wa Wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ili kuimarisha misingi ya demokrasia, uwazi, na ushirikishwaji wa wanachama wengi zaidi katika mchakato wa kura za maoni.

Baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ni pamoja na:

  1. Mchakato wa uchujaji na uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi wa majimbo, na udiwani wa kata/wadi.
  2. Mchakato wa uchujaji na uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi, na udiwani wa viti maalum wanawake.
  3. Upanuzi wa idadi ya wajumbe wa vikao vya chama na jumuiya zake watakaopiga kura za maoni.

Katika mabadiliko hayo, wajumbe wa mikutano mikuu maalumu ya jumuiya za UWT, UVCCM, na WAZAZI sasa watahusika moja kwa moja katika kura za maoni kwa wagombea wa viti maalum.

Aidha, CCM imeweka ukomo wa vipindi viwili vya miaka mitano kwa nafasi za ubunge/uwakilishi na udiwani wa viti maalum wanawake, ambao utaanza kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030.

Kauli Mbiu Mpya ya Uchaguzi Mkuu 2025

Katika kikao hicho, CCM pia imepitisha kauli mbiu rasmi kwa ajili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 inayosema:

“KAZI NA UTU, TUNASONGA MBELE”

Kauli mbiu hiyo inaakisi dhamira ya chama kuendeleza juhudi za maendeleo jumuishi, mshikamano wa kitaifa, na ustawi wa jamii yenye misingi ya utu.

Kwa mabadiliko haya, CCM inalenga kuimarisha demokrasia ndani ya chama, kupanua uwakilishi wa wanachama katika uteuzi wa wagombea, na kuhakikisha uongozi wenye uwajibikaji na maadili kwa maendeleo ya taifa.