Paul Kagame na Félix Tshisekedi Wakutana Qatar kwa Hatua Muhimu ya Kusitisha Uhasama

Kagame and Tshisekedi met in Qatar

Wakati mataifa ya Magharibi yameendelea kuwekea vikwazo bila suluhisho la kweli kwa amani, Qatar imefanikiwa kufungua njia mpya ya mazungumzo kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Paul Kagame na Félix Tshisekedi Wakutana Qatar kwa Hatua Muhimu ya Kusitisha Uhasama tarehe 18 Machi 2025 mjini Doha. Rais wa Rwanda, Paul Kagame na mwenzake wa DRC, Félix Tshisekedi, walikutana Doha kwa jitihada kubwa za kidiplomasia zinazolenga kumaliza mzozo katika eneo la mashariki mwa DRC.

Mazungumzo hayo yaliandaliwa na Emir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, na yalilenga kufufua juhudi za amani zilizosimama huku viongozi hao wakirejelea ahadi ya kusitisha mapigano.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, mkutano huo ulikuwa hatua muhimu kuelekea uthabiti wa kikanda.

“Qatar itaendelea kusaidia juhudi za mazungumzo na ushirikiano kati ya pande zote ili kuhakikisha amani ya kudumu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na ukanda mzima” ilisema wizara hiyo katika taarifa yake.

Mazungumzo haya yaliendeleza juhudi zilizowahi kufanyika kupitia mchakato wa amani wa Ruanda na Nairobi, ambao kwa sasa umeunganishwa na mpango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Viongozi hao walithibitisha tena ahadi ya kusitisha mapigano mara moja na bila masharti, kama walivyokubaliana katika mkutano wa Dar es Salaam mwezi Februari.

“Mazungumzo yaliyofanyika Doha yanaonesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha utulivu na usalama katika eneo hilo. Mwaliko wa Emir kwa viongozi hawa wawili unaonesha nafasi ya Qatar kama msuluhishi wa upande wa kati katika changamoto za kisiasa za kikanda,” ilisema Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar.

Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje – Qatar kuhusu kukutana kwa Marais hawa

Mkutano huu unakuja wakati mgogoro kati ya Rwanda na DRC ukizidi kuwa mbaya, huku serikali ya Congo ikiendelea kuishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 walioteka miji muhimu ya Bunagana na Kitshanga katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Serikali ya DRC imesisitiza kuwa kundi hilo, lililorejea vitani mwishoni mwa 2021, ni chombo cha maslahi ya Rwanda katika eneo hilo—madai ambayo Kigali imekanusha vikali.

Uhusiano kati ya Kagame na Tshisekedi umedorora kwa kiwango kikubwa katika miaka ya hivi karibuni, huku kila mmoja akimlaumu mwenzake kwa kuchochea mzozo huo.

Hapo awali, Tshisekedi alikataa kuzungumza moja kwa moja na Kagame, akimfananisha na Adolf Hitler na kudai kuwa Rwanda lazima iache kuunga mkono M23 kabla ya mazungumzo yoyote. Hata hivyo, kutokana na shinikizo la kikanda na hali mbaya ya usalama, inaonekana msimamo wake umeanza kubadilika.

Kwa upande mwingine, Rwanda imekuwa ikikabiliwa na vikwazo vya kimataifa kufuatia tuhuma za kuhusika kwake kwenye mzozo wa DRC. Marekani, Umoja wa Ulaya, na mataifa mengine ya Magharibi yameweka vikwazo kwa maafisa wa Rwanda na kusitisha misaada, lakini Qatar imechukua njia tofauti katika kutatua mkwamo huu wa kisiasa.

Licha ya juhudi hizi, waasi wa M23 wanaendelea kupanua maeneo wanayoyadhibiti, hali inayoathiri zaidi juhudi za kurejesha amani.

Jukumu la Qatar katika kuandaa mkutano huu linaonesha jaribio la kutafuta suluhisho la kweli kwa mzozo huo. Ingawa hakuna makubaliano ya mwisho yaliyotangazwa, hatua ya Kagame na Tshisekedi kukutana baada ya miezi kadhaa inaweza kufungua milango kwa mazungumzo zaidi ya kidiplomasia.