Jezi namba 39 kwa Bruno ni namba ya taxi aliyoendesha baba yake

Nahodha wa klabu ya Newcastle United, Bruno Guimaraes, amefichua siri ya namba ya jezi yake (39) akisema kuwa ni namba iliyomsaidia mambo mengi katika ukuaji wake kisoka, huku akimtaja baba yake kuwa ndio muhusika mkuu wa namba hiyo.

“Watu wanahisi namba 39 haipendezi katika jezi, lakini kwangu mimi hii namba imenisaidia sana nilipokuwa kijana mdogo.

“Baba yangu mzazi alikuwa na taxi iliyokuwa inabeba abiria katika jiji la Rio de Janeiro, namba #039 ilitumika kuitambulisha taxi hiyo. 

“Baba alipambana sana ili nile, nivae na kunisaidia kutimiza ndoto zangu za soka hivyo siwezi kuisahau namba hii,” alinukuliwa Bruno katika mahojiano baada ya fainali ya Carabao Cup huku akibubujikwa na machozi.

Guimarães alijiunga na Newcastle United mwaka 2022 akitokea Olympique Lyonnais, na tangu wakati huo amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi hicho. 

Licha ya nafasi yake kama kiungo mkabaji, amefanikiwa kufunga mabao tisa katika mechi 41 alizocheza kwa klabu hiyo, akionyesha uwezo wake mkubwa wa kupiga pasi na kudhibiti mchezo.  

Kwa kuvaa jezi namba 39, Guimarães anawakilisha hadithi ya kujitolea na shukrani kwa familia yake, hasa baba yake, ambaye alifanya kazi kwa bidii ili kumsaidia kufikia ndoto yake ya kuwa mchezaji wa soka wa kimataifa. 

Hii inaonyesha jinsi wachezaji wanavyoweza kutumia namba za jezi zao kuonyesha heshima na kuthamini wale waliowasaidia katika safari yao ya mafanikio.