Soko la hisa nchini Japan limefungua likiwa limeshuka, kufuatia wasiwasi wa wawekezaji kuhusu mabadiliko ya ghafla ya sera za kibiashara za Rais wa Marekani, Donald Trump.
Kupitia taarifa kwa baraza lake la mawaziri hapo jana, Rais Trump alieleza kuwa kipindi hiki kigumu hakiepukiki, lakini alisisitiza kuwa wawekezaji wameonyesha matumaini na kuunga mkono hatua anazochukua kulinda uchumi wa Marekani.
Wakati huo huo, thamani ya sarafu ya Dola ya Marekani imeporomoka dhidi ya sarafu za Ulaya, huku bei ya mafuta ikishuka kwa karibu asilimia nne, hali inayochochewa zaidi na mvutano unaoendelea kati ya Marekani na China kuhusu ushuru wa kibiashara.
Katika ishara ya kuimarika kwa vita vya ushuru kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu kubwa kiuchumi, vyombo vya habari vya serikali ya China vimeanza kuhimiza raia wake kuwa tayari kwa changamoto za kiuchumi zitakazotokana na hatua za kisasi zinazochukuliwa na Marekani.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karoline Leavitt, akizungumza na kituo cha habari cha Fox News, alisema kuwa sera ya sasa ya Marekani inalenga kulinda maslahi ya kitaifa kwa kuiweka Marekani mbele kiuchumi na kurejesha ajira kutoka nje ya nchi.
“Sera ya Ikulu hii ni kuiweka Marekani mbele na kurejesha ajira,” alisema Leavitt. “Hatutaruhusu tena bidhaa za bei ya chini kutoka China kuingia kwa wingi katika soko letu huku wao wakizuia bidhaa zetu kuingia kwao.”
Leavitt aliongeza kuwa Marekani haiwezi kuendelea kustawi kiuchumi ikiwa itaendelea “kuinyanyua na kuipa nguvu China” kwa kuruhusu uagizaji mkubwa wa bidhaa kutoka taifa hilo la Asia.
Katika hatua ya hivi karibuni, Ikulu ya Marekani imetangaza kuwa ushuru mpya kwa bidhaa kutoka China utaongezeka hadi asilimia 145, ikilinganishwa na asilimia 125 iliyotangazwa awali. Kwa mujibu wa maafisa wa Ikulu, kiwango hicho kipya ni muendelezo wa ongezeko la asilimia 20 lililowekwa wiki chache zilizopita dhidi ya bidhaa za China.
Wachambuzi wa masoko ya fedha wanasema hali hii inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa biashara za kimataifa, huku wawekezaji wakichukua tahadhari zaidi kutokana na kutotabirika kwa mwelekeo wa sera za Marekani.
Leave a Reply