kiongozi wa kijeshi aliyeongoza mapinduzi ya Agosti 2023 nchini Gabon, Jenerali Brice Oligui Nguema ameshinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Urais uliofanyika Jumamosi, akipata asilimia 90.35 ya kura zote zilizopigwa.
Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hermann Immongault, yanaonyesha uungwaji mkono mkubwa wa wananchi kwa Oligui, ambaye alichukua madaraka baada ya kumng’oa madarakani Rais Ali Bongo Ondimba, ambaye familia yake ilidumu madarakani kwa zaidi ya miaka 50.
Oligui, ambaye ni jenerali wa zamani wa jeshi, alianzisha kampeni kabambe ya kuwania urais kwa kutembelea maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, akiwahutubia wananchi moja kwa moja, jambo lililosaidia kukuza umaarufu wake na kuimarisha uungwaji mkono wa kisiasa.
Katika kampeni zake, Oligui aliahidi kufanya mageuzi ya kiuchumi kwa kupanua vyanzo vya mapato ya taifa, kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira na kupunguza kiwango cha umaskini ambacho kimekuwa kikiiandama nchi hiyo kwa muda mrefu.
Ushindi huu unaashiria mwanzo mpya wa uongozi nchini Gabon, huku macho ya raia na jumuiya ya kimataifa yakielekezwa kwa Oligui kuona kama atatimiza ahadi alizotoa na kuleta mabadiliko ya kweli.
Leave a Reply